MAKAMU WA RAIS AIPAISHA AJENDA YA GESI MTWARA

  


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi amesema uwekezaji wa Serikali katika mradi wa bomba la gesi kutoka Ntorya kwenda Madimba, mkoani Mtwara, unaweka msingi wa kuongeza mchango wa gesi asilia katika uchumi wa taifa kupitia uzalishaji wa umeme, maendeleo ya viwanda na upanuzi wa matumizi yake katika usafiri na majumbani.

 Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo unaogharimu takribani Sh bilioni 119 za fedha za ndani, Makamu wa Rais ameipongeza Wizara ya Nishati na timu ya utekelezaji Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC)  kwa hatua iliyofikiwa, huku akieleza umuhimu wa uwekezaji huo katika kupanua upatikanaji wa nishati kwa shughuli za kiuchumi na kijamii.

 Amesema kuunganishwa kwa kisima cha gesi cha Ntorya na Kituo cha Kuchakata Gesi cha Madimba kutaongeza uwezo wa kusambaza gesi kwa matumizi mbalimbali nchini, yakiwemo kuzalisha umeme na kuendesha viwanda.

 Pia, Makamu wa Rais amesema mradi huo utapanua fursa za matumizi ya gesi katika usafiri na kupikia na hivyo kutekeleza kwa Vitendo agenda ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya matumizi ya nishati safi kupikia.  

 Ziara hiyo imeweka mbele ajenda ya Serikali ya kutumia rasilimali za ndani kuimarisha uchumi, huku ikiibua matarajio ya wananchi kuhusu namna uwekezaji katika gesi utakavyoendelea kuboresha huduma na kuongeza fursa katika maeneo yao.

 Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TPDC CPA Mussa Mohammed Makame wakati wa ukaguzi wa shughuli ya ulazaji wa bomba la Ntorya–Madimba amesema zoezi limekamilika kwa asilimia 78 , huku kazi za uunganishaji wa mwisho na miundombinu mingine ya mradi zikiendelea. Matarajio mradi huo utakamilika Februari 2027.

 Kisima cha Ntorya kilichimbwa mwaka 2012. Kuunganishwa kwake na Madimba sasa kunasogeza mbele hatua ya kutumia rasilimali hiyo kukidhi mahitaji ya nishati na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya taifa.

 






Katika ziara hiyo, Mbunge wa Mtwara Vijijini, Arif Suleiman Premji, amesema wananchi wameanza kuona baadhi ya manufaa ya uwekezaji katika sekta hiyo kupitia miradi ya huduma za jamii.

 Ametaja takribani Sh bilioni 4.7 zilizotolewa kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali, ikiwemo vituo vya afya na miundombinu ya elimu, hatua inayochangia kuimarisha huduma kwa wananchi.

 Mradi wa Ntorya–Madimba ni sehemu ya juhudi za Serikali, kupitia Wizara ya Nishati na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kwa kushirikiana na wawekezaji, kuendeleza utafutaji, uzalishaji na usafirishaji wa gesi asilia nchini.

 Mikoa ya Lindi na Mtwara ina nafasi muhimu katika utekelezaji wa ajenda hiyo kutokana na rasilimali zilizogunduliwa na maeneo yanayoendelea kufanyiwa utafiti.

 Kwa mujibu wa taarifa ya miradi hiyo, hadi Agosti 2026 Tanzania ilikuwa imegundua gesi asilia yenye jumla ya futi za ujazo trilioni 57.54, huku sehemu kubwa ikiwa katika kina kirefu cha Bahari ya Hindi, nje ya Pwani ya Mikoa hiyo.

 Shughuli zinazoendelea zinajumuisha uzalishaji wa gesi katika maeneo ya Mnazi Bay na Songo Songo, uendelezaji wa gesi ya Ntorya na ujenzi wa bomba la Ntorya–Madimba. Aidha, majadiliano yanaendelea kuhusu mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia kuwa kimiminika (LNG), unaotarajiwa kutekelezwa Likong’o, mkoani Lindi.

 Sambamba na uwekezaji huo, usambazaji wa gesi kwa matumizi ya kupikia unaendelea kupanuliwa katika mikoa ya Lindi na Mtwara, ikiwa ni sehemu ya kuwafikishia wananchi manufaa ya rasilimali hiyo.

 Ukaguzi wa Makamu wa Rais katika mradi wa Ntorya–Madimba umeweka uzito katika nafasi ya gesi asilia kuchangia maendeleo ya Taifa, huku mahitaji yaliyowasilishwa na wananchi yakibainisha matarajio yao ya kuona uwekezaji huo ukipanua huduma bora na fursa za kiuchumi.

 

No comments