Bunge la Tanzania kuadhimisha miaka 100 kwa staili ya aina yake


 


BUNGE la Tanzania linatarajia kuadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwa chombo cha kwanza cha kutunga sheria Tanganyika, huku kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika Januari 28, 2027 katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma.

 Maadhimisho hayo yataambatana na shughuli mbalimbali ikiwamo ujenzi wa Mnara wa Kumbukumbu ya Miaka 100 ya Bunge na kuendesha Bunge la Vijana kwa lengo la kuwajengea vijana uelewa na kuwawezesha kushiriki shughuli za kibunge.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha Mkutano wa Tano wa Bunge la 13 jana jijini hapa, Spika wa Bunge, Mussa Zungu alisema mwaka 2026 ni wa kihistoria kutokana na kutimia miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Kutunga Sheria Tanganyika (LEGCO).

Zungu alisema Machi 19, 1926 Bunge la Uingereza lilipitisha sheria iliyojulikana kama Baraza la Kutunga Sheria Tanganyika (Amri ya Baraza ya 1926), iliyoweka msingi wa kuanzishwa kwa baraza hilo.

Alifafanua kuwa kikao cha kwanza kilifanyika Desemba 7, 1926 chini ya Gavana wa Tanganyika wa wakati huo, Sir Donald Cameron, kikiwa na wajumbe 20 walioteuliwa na gavana, ambao 19 walikuwa Wazungu na mmoja Mhindi.

Katika mfumo huo wa kikoloni, sheria zilizopitishwa na baraza hilo ziliwasilishwa Uingereza kwa ajili ya kupata idhini ya mfalme.

Zungu alisema katika kipindi cha miaka 100, bunge limepitia mabadiliko, changamoto na mafanikio mbalimbali yaliyolifanya kuwa taasisi muhimu katika maendeleo ya taifa.

Alisema maadhimisho hayo yana kaulimbiu isemayo, “Miaka 100 ya Bunge, Historia Yetu, Dira Yetu,” inayosisitiza umuhimu wa kutumia historia kujenga mustakabali wa taasisi hiyo.

Alieleza Desemba 7, 2026 ndiyo siku ya kutimia miaka 100 tangu kikao cha kwanza cha baraza hilo lakini kilele kimepangwa Januari 28, 2027 kwa kuwa Desemba wabunge watakuwa majimboni kutekeleza majukumu yao kwa wananchi.

No comments