TANZANIA YALENGA MAPINDUZI YA UCHUMI KUPITIA UMEME NA NISHATI YA UHAKIKA
Serikali ya
Tanzania imeeleza kuwa inalenga kufanya umeme na nishati ya uhakika kuwa msingi
wa mapinduzi ya uchumi yatakayochochea ukuaji wa viwanda, uwekezaji, ajira na
maendeleo ya Taifa kuelekea mwaka 2050, huku ikilenga kuongeza uwezo wa
uzalishaji wa umeme hadi zaidi ya megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030/31.
Hayo
yameelezwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), kwa niaba ya
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, baada ya kuongoza Mkutano wa 35
wa Bodi ya Magavana wa Taasisi ya Kujenga Uwezo Afrika (The African Capacity
Building Foundation – ACBF), unaofanyika sambamba na Mkutano wa Afrika wa
Taasisi za Tafiti na Majadiliano ya Sera (Africa Think Tank Summit – ATTS),
mjini Cotonou, Jamhuri ya Benin.
Mhe.
Luswetula alisema Tanzania inatambua kuwa upatikanaji wa umeme na nishati ya
uhakika ni kichocheo muhimu cha maendeleo ya kiuchumi, hususan katika kuvutia
uwekezaji, kupanua uzalishaji viwandani, kuimarisha miundombinu na kuboresha
maisha ya wananchi.
Aliongeza
kuwa upatikanaji wa nishati ya kutosha ni miongoni mwa nguzo zitakazosaidia kufanikisha
kutimiza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 ya kufikia uchumi wa
dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050, na wastani wa pato la mtu
mmoja kufikia takriban dola za Marekani 7,000.
“Tanzania
tupo tayari kwa mapinduzi ya kiuchumi kwa sababu malengo yetu na nia yetu ni
kuhakikisha tunakuwa na umeme na nishati ya kutosha kwa ajili ya maendeleo ya
wananchi, maendeleo ya Taifa na kukuza uchumi wetu,” alibainisha Mhe.
Luswetula.
Alisema
Serikali inaendelea kuimarisha uzalishaji na usambazaji wa umeme ili kukidhi
mahitaji ya sasa na yajayo, yanayochangiwa na ongezeko la shughuli za kiuchumi,
uwekezaji mpya na upanuzi wa viwanda nchini.
“Lengo letu
ni kufikia zaidi ya megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030/31. Tunajua kuwa ili
tuweze kuanzisha viwanda vingi, kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi, ni lazima
tuwe na umeme wa kutosha,” alisema Mhe. Luswetula.
Alieleza kuwa
upatikanaji wa umeme wa kutosha utawezesha kuanzishwa kwa viwanda vingi,
kuongeza uzalishaji na kusaidia utekelezaji wa miradi ya kimkakati, ikiwemo
Reli ya Kisasa (SGR), inayotarajiwa kufika Mwanza, Kigoma na maeneo mengine
nchini.
Alibainisha
kuwa upatikanaji wa umeme wa uhakika utasaidia kuweka mazingira bora kwa
wawekezaji wapya na waliopo kupanua shughuli zao, kuongeza uzalishaji na
kutumia fursa zinazotokana na ukuaji wa uchumi.
Mhe.
Luswetula alisema kuwa sera zinazotekelezwa sasa chini ya uongozi wa Mheshimiwa
Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zimeendelea
kuweka mazingira bora kwa wawekezaji na wafanyabiashara waliopo nchini, pamoja
na wale wanaotaka kuwekeza kwa mara ya kwanza.
Mhe.
Luswetula alisisitiza kuwa juhudi za Serikali hazilengi kuongeza uzalishaji wa
umeme pekee, bali pia kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi na kuchangia
maendeleo ya shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha,
alisema Serikali inaendelea kupanua upatikanaji wa umeme katika maeneo ambayo
bado hayajafikiwa kikamilifu, huku zaidi ya vitongoji 9,000 vipya vikitarajiwa
kupata umeme katika awamu inayoendelea.
Mkutano wa 35
wa Bodi ya Magavana wa Taasisi ya Kujenga Uwezo Afrika (ACBF) umejikita katika
kujadili masuala ya nishati, kuanzia uzalishaji na usambazaji hadi kuhakikisha
wananchi wananufaika na upatikanaji wa nishati hiyo.
Katika
mkutano huo, Tanzania imejadiliana na washiriki kutoka nchi nyingine za Afrika
kuhusu kuhakikisha nchi za Afrika zinakuwa na utoshelevu wa nishati na
kuanzisha viwanda vingi, huku umeme ukiwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi
katika nchi hizo.

Post a Comment