SERIKALI KUENDELEA KUFANYIA KAZI TAARIFA YA CAG-DKT MWIGULU




* Asema hatua kali zitachukuliwa kwa wote watakaobainika kuhusika na ubadhirifu

 

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali imeendelea kuyafanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na hatua kali zitachukuliwa kwa  watakaobainika kufanya ubadhirifu.

“Niwakumbushe Maafisa Masuuli na watendaji wote wa Serikali kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za matumizi ya fedha za umma kwa mujibu wa mipango na bajeti ili kuepusha hoja za ukaguzi na upotevu wa fedha za umma. Niwakumbushe watumishi wote kuwa fedha za umma ni kodi za wananchi.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Novemba 6, 2026) wakati akiahirisha Mkutano wa Tano wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania jijini Dodoma. Amesema Serikali itazingatia mapendekezo yote yaliyotolewa na Bunge kupitia maazimio na hoja zilizowasilishwa. 

Amesema Waheshimiwa Wabunge wamechangia kwa hisia kali wakieleza namna walivyo na uchungu na rasilimali za Taifa letu. “Wabunge katika Bunge lako Tukufu wanawawakilisha vyema wananchi wa Tanzania, hususan katika usimamizi wa rasilimali na kuisimamia Serikali.” 

“Nitumie nafasi hii kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Serikali itayafanyia kazi matokeo ya taarifa za ukaguzi, kama ambavyo Mheshimiwa Rais amekwisha kuelekeza kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kutopepesa macho anapofanya ukaguzi.” 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema tarehe 30 Oktoba, 2026, itabaki kuwa siku ya kihistoria kwa Taifa letu, ambapo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua Mji wa Serikali uliopo Mtumba, jijini Dodoma, hivyo ametumia fursa hiyo kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa hatua hiyo kubwa. 

Kufuatia uzinduzi huo wa Mji wa Serikali, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ameelekeza shughuli za Serikali zifanyike Dodoma, Makao Makuu ya nchi kwa kuwa ofisi zimekamilika, hivyo waache kuendesha ofisi sambamba za Dodoma na Dar es Salaam. “Makao Makuu ya nchi yetu ni Dodoma.” 

Pia, Waziri Mkuu amezielekeza wizara na taasisi zote zitekeleze maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa siku ya uzinduzi wa Mji wa Serikali na shughuli zote zifanyike katika majengo ya Mji wa Serikali, waache kuendelea kutumia majengo ya kukodi kwa kuwa majengo ya Serikali yamekamilika. 

Aidha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kushirikiana na wadau wa usafirishaji, ihakikishe usafiri wa umma unapatikana kwenda Mji wa Serikali ili kuwawezesha wananchi kufika kupata huduma

No comments