TATIZO LA YANGA NI UONGOZI NA MFUMO, SIO KOCHA
Ligi Kuu Tanzania Bara inaingia katika mzunguko wa 10 huku baadhi ya klabu zikiwa zimeshaingia kwenye maamuzi ya kuwafuta kazi makocha wao kutokana na mwenendo wa kusuasua. Miongoni mwa makocha waliokumbwa na rungu hilo ni pamoja na Juma Kaseja wa Kagera Sugar, Etienne Ndayiragije wa TRA United, na Manqoba Mngqithi wa Yanga.
Kufukuzwa kwa Manqoba kulichochewa na matokeo mabaya ya hivi karibuni, ikiwemo kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya watani wao wa jadi, Simba, pamoja na matokeo ya suluhu dhidi ya TRA United.
Hata hivyo, ukweli ulio wazi ni kwamba kuporomoka kwa viwango vya Yanga hivi karibuni si matokeo ya udhaifu wa kocha, bali ni mchanganyiko wa matatizo mazito ya kinidhamu, kiufundi na kiutawala yanayoendelea ndani na nje ya uwanja.
Moja ya changamoto kubwa za kiufundi zinazoikabili klabu hiyo ni uchovu wa wachezaji kutokana na ratiba ngumu za mashindano na majukumu ya timu za taifa, kukosekana kwa umakini katika umaliziaji wa nafasi zinazotengenezwa, pamoja na kupotea kwa muunganiko thabiti uwanjani uliokuwepo katika misimu iliyopita. Badala ya uongozi kutatua matatizo hayo ya kimfumo, umekuwa ukiendeleza utamaduni wake wa kukimbilia kufukuza benchi la ufundi kila matokeo yanapoyumba.
Udhaifu mkubwa wa kiutawala unaonekana wazi katika maamuzi ya usajili na mauzo ya wachezaji. Uamuzi wa kumuuza Allan Okello kwenda Klabu ya AS FAR Rabat ya Morocco na badala yake kumrejesha Stephane Aziz Ki kutoka Al-Ittihad ya Libya ulikuwa makosa makubwa ya kiufundi.
Katika kipindi kifupi alichohudumu Yanga, Okello alifunga mabao 14 na kutoa pasi saba za mabao zilizosaidia kutwaa ubingwa. Kwa upande mwingine, Aziz Ki alirejeshwa akiwa na takwimu za chini, ambapo msimu wa 2024/25 akiwa Wydad Casablanca alicheza mechi nane tu na kufunga bao moja, huku akiwa Al-Ittihad ya Libya akifunga mabao manane na pasi tatu za mabao katika ligi yenye ushindani mdogo kulinganisha na ya kwetu.
Kosa jingine la kibiashara na kiufundi lilikuwa kumuuza mshambuliaji Laurindo Aurélio 'Depu' kwenda Petro de Luanda ya Angola na kumsajili Cheikh Ibrahima Touré akiwa mchezaji huru. Hatua hii ilileta faida za kifedha katika mifuko ya klabu lakini haina tija ya kiwanjani, kwani Depu alifunga mabao 14 na kutoa pasi tatu za mabao ndani ya miezi saba pekee. Licha ya Yanga kutwaa Ngao ya Jamii na kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, usajili wa wachezaji hao wa kigeni bado haujaonyesha makali yaliyototarajiwa.
Ni wazi kuwa matatizo ya Yanga hayawezi kumalizika kwa kumfukuza kocha pekee. Uongozi unapaswa kujitathmini na kuacha kukimbilia kivuli cha benchi la ufundi, bali utatue changamoto za msingi za kimaamuzi, nidhamu na sera za usajili ili kuirejesha timu hiyo katika ubora wake.

Post a Comment