MwanaFA afurahishwa na ushindani wa watayarishaji muziki




NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ amesema amefurahishwa na ushindani unaoendelea kati ya watayarishaji wa muziki wa kizazi kipya nchini, akieleza kuwa hali hiyo inachochea ukuaji na maendeleo ya tasnia ya muziki.

Katika mahojiano yake na Jambo Fm, alisema ushindani unaoonekana kati ya watayarishaji Salmin Maengo ‘S2Kizzy’ na Thabit Mango ‘Mr T-Touch’ kuhusu nani ni bora ni jambo zuri kwa kuwa unawapa wasanii nafasi ya kuonesha uwezo wao kupitia kazi wanazozalisha.  

Akizungumza kuhusu hali hiyo, Mwana FA alisema anafurahia kuona watayarishaji wakijiamini na kutangaza uwezo wao na kusisitiza kuwa ni vizuri zaidi pale wanapoweza kuthibitisha kauli zao kupitia kazi walizozifanya.

Alisema ubora wa mtayarishaji hutegemea aina ya muziki ambao msanii anahitaji, akitoa mfano kuwa mwanamuziki Ali Kiba anaweza kumtaja Sweetbert Mwanula ‘Abbah Process’ kuwa mtayarishaji anayemfaa, wakati Diamond Platnumz anaweza kumtaja S2Kizzy kutokana na mahitaji yao ya kimuziki.

Mwana FA alisema amewahi kufanya kazi na watayarishaji hao pamoja na wengine, hivyo anaelewa uwezo wa kila mmoja na namna wanavyoweza kukidhi mahitaji tofauti ya wasanii. 

Kuhusu suala la mirabaha, alisema wasanii wanapaswa kufuata taratibu zilizowekwa ili kupata stahiki zao, akibainisha kuwa hata yeye amewahi kukumbana na changamoto ya kuchelewa kupata mirabaha, licha ya kuwa sehemu ya serikali na kufahamu baadhi ya taratibu zinazohusika.

Alisisitiza kuwa wasanii ambao hawajapata mirabaha yao wanapaswa kufika katika ofisi ya hakimiliki ili kusaidiwa kubaini chanzo cha tatizo na hatua zinazopaswa kuchukuliwa na kufafanua kuwa huenda baadhi yao wana malipo ya miaka mingi ambayo bado hawajayafuatilia. 

Alisema serikali ina wajibu wa kuhakikisha wabunifu wanalipwa haki zao kwa kazi wanazozalisha ili muziki uweze kuwa chanzo cha kipato na kuwawezesha kunufaika na kazi zao kupitia njia mbalimbali zinazopatikana.


No comments