UWEKEZAJI WA BILIONI 3.17 WAWAONDOLEA SONGEA DC ADHA YA KUSAFIRI KUSAKA MATIBABU



Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma wameanza kuondokana na adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya, kufuatia kuanza kutolewa kwa huduma za matibabu, uchunguzi na upasuaji katika Hospitali ya Wilaya ya Songea. 

Hatua hiyo imewezeshwa na uwekezaji mkubwa wa zaidi ya Shilingi bilioni 3.17 uliofanywa na Serikali katika kuboresha miundombinu, vifaa tiba na upatikanaji wa huduma za afya katika hospitali hiyo.

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Sakina Komesha, anaeleza kuwa hivi sasa wamejikamilisha na vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa X-ray, pamoja na kutoa huduma za upasuaji, macho na meno, ambazo awali ziliwalazimu wananchi kufuata huduma hizo katika hospitali kubwa za mbali. 

Dkt. Komesha anaongeza kuwa hospitali hiyo pia inatoa huduma za uzazi na upasuaji wa dharura kwa kina mama wajawazito, hatua inayosaidia kuokoa maisha ya mama na mtoto kwa kuondoa ucheleweshaji uliokuwa ukijitokeza zamani.

Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Dkt. Zaituni Hamza, anabainisha kuwa kuongezwa kwa miundombinu na wataalamu kumeongeza uwezo wa hospitali kutoa huduma mbalimbali, ikiwemo uchunguzi wa magonjwa na matibabu kwa watoto, jambo linalowagusa moja kwa moja wananchi wa maeneo ya mbali.






Akishirikisha uzoefu wake, Fatuma Umbala, mkazi wa Kijiji cha Nambendo, Kata ya Mpitimbi, anasema alipomfikisha mgonjwa wake hospitalini hapo kujifungua, alipokelewa vizuri na wahudumu wa afya waliomhudumia kwa haraka na kuendelea kumfuatilia hadi alipopata nafuu. Pamoja na kuridhishwa na huduma hizo, Fatuma ametoa wito kwa Serikali kuendelea kuongeza watumishi hospitalini hapo ili kuendana na kasi ya wananchi wengi wanaofika kupata matibabu kila siku.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Elizabeth Gumbo, anasema uwekezaji huo umeleta afueni kubwa kwa wananchi, huku ujenzi wa nyumba za watumishi jirani na hospitali ukisaidia kuweka mazingira mazuri ya utendaji kazi na kuimarisha upatikanaji wa huduma wakati wote.

Maboresho hayo yanazidi kudhihirisha umuhimu wa kuimarisha hospitali za wilaya nchini katika kupunguza gharama za usafiri, kurahisisha matibabu na kuokoa maisha ya wananchi kwa kutoa huduma kwa wakati.

No comments