THE MIDNIGHT BRIDE KUONESHWA KWA WARUSI
FILAMU ya ‘The Midnight Bride’ ya mtayarishaji Doreen Kilimbe, iliyoongozwa na Clerick Morgeni inatarajiwa kuoneshwa Oktoba 30, mwaka huu katika Kituo cha Sayansi na Utamaduni cha Urusi nchini Tanzania (RCSC) mkoani Dar es Salaam.
Filamu hiyo itaoneshwa kuanzia saa 12:00 jioni na Bodi ya Filamu Tanzania kwa kushirikiana na Kituo cha Sayansi na Utamaduni cha Urusi.
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, Dk Gervas Kasiga alisema onesho hilo ni sehemu ya jitihada za kuendeleza na kukuza utamaduni wa kutazama, kuthamini na kuunga mkono kazi za filamu zinazozalishwa na wabunifu wa Tanzania.
“The Midnight Bride ni filamu ya Kitanzania na ni kazi ya Mtanzania. Karibu tushiriki pamoja katika kuienzi na kuiunga mkono tasnia ya filamu Tanzania” alisema Dk Kasiga.
Onesho hilo limekuja baada ya Tanzania na Urusi kukubaliana kuendeleza programu ya pamoja ya kuonesha filamu za Kitanzania na za Kirusi.
Mpango huo unalenga kutoa fursa kwa watazamaji na wadau wa filamu kufahamu kazi za filamu kutoka Tanzania na Urusi na kuwa jukwaa la kukuza utamaduni, kubadilishana uzoefu na kuimarisha mahusiano ya kiutamaduni kupitia sanaa ya filamu.

Post a Comment