KADERES PLC, CRDB WATAMBULISHA MRADI WA BIASHARA YA HEWA YA KABONI RUVUMA
Kampuni ya KADERES PLC kwa kushirikiana na Benki ya CRDB wametambulisha mradi wa biashara ya hewa ya kaboni mkoani Ruvuma, utakaowawezesha wakulima kuingia kwenye kilimo biashara kupitia kilimo mseto.
Uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa Songea Club, Manispaa ya Songea, ambapo katika awamu ya kwanza, mradi unatarajiwa kusajili wakulima 60,000 kutoka halmashauri mbalimbali za mkoa huo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Mhe. Kisare Makori, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ahmed Abbas, amesema mradi huo ni fursa muhimu ya biashara ya hewa ya kaboni kupitia mashamba ya chakula na biashara.
Makori ameitaka KADERES PLC kutoa elimu ya kina kwa wadau na kuandaa ziara za mafunzo ili wakulima wajifunze fursa na changamoto za mradi, kisha kujiunga kwa hiari.
Kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Katibu Tawala Msaidizi wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Yusuph Jerico Mwakatobe, amesema mkoa uko tayari kushiriki, na shughuli za kupanda miti zitakuwa sehemu ya juhudi za mkoa na taifa za kutunza mazingira.
Naye Mkurugenzi wa KADERES PLC, Leonard Kachebonaho, amesema lengo kuu ni kuwasaidia wakulima kuwekeza katika kilimo mseto kitakachowawezesha kustahimili changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Akibainisha kuwa wakulima watakaosajiliwa wataanza kunufaika kupitia kilimo cha kikaboni na kupata ruzuku kwa kuingizwa kwenye mfumo rasmi wa biashara ya hewa ya kaboni.
Kwa upande wake, Meneja wa mifumo ya kidigitali kilimo biashara CRDB, Allawi Mdee, amesema benki hiyo imetenga shilingi bilioni 9 kwa ajili ya kusajili wakulima wadogo. Pia, amesisitiza kuwa wakulima watakaosajiliwa hawatalazimika kutoa fedha kwa ajili ya usajili, kwani gharama zote zimeshughulikiwa na benki.
Post a Comment