MASWALI NA MAJIBU YA SERIKALI BUNGENI OKT 30: TEKNOLOJIA, ELIMU NA AFYA




KUIMARISHA SEKTA YA AFYA - GEITA MJINI

MHESHIMIWA ENG. CHACHA MWITA WAMBURA (GEITA MJINI) Atauliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha sekta ya Afya kwa kuongeza Vituo vya Afya, Madaktari, Wauguzi na Vifaa tiba - Geita Mjini.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (TAMISEMI) Atajibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendeleta kuimalisha huduma za afya hususani Ngazi ya Afya ya Msingi kwa kujenga/kukarabati miundombinu ya afya, kuajiri watumishi wa Kada za Afya pamoja na kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa na Vifaa Tiba.

Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2024/25 na 2025/26 Serikali imeajiri jumla ya watumishi wa Kada ya Afya 11,198 ambapo watumishi wa Kada ya Uuguzi walioajiriwa walikuwa 6,450 na Halmashauri ya Mji wa Geita ilipangiwa jumla ya watumishi wa afya 109.

Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2026/27 Serikali imetenga shilingi bilioni 56.25 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa Hospitali na shilingi bilioni 23.37 kwa ajili ya ukamilishaji wa vituo vya afya 111 kote nchini. Aidha, halmashauri ya Mji wa Geita imetengewa shilingi milioni 170 kwa ajili ya ukamilishaji wa vituo vya Afya.

Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha 2026/27 Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 405 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba, ambapo Mkoa wa Geita umetengewa shilingi bilioni 7.28 na Manispaa ya Geita imetengewa kiasi cha shilingi bilioni 1.09.

UHITAJI WA WODI YA WATOTO KITUO CHA AFYA CHA MJIMWEMA SONGEA

MHESHIMIWA MARIAMU MADALU NYOKA (VITI MAALUM) Atauliza:-

Je, lini Serikali itajenga Wodi ya Watoto katika Kituo cha Afya cha Mjimwema kilichopo Manispaa ya Songea.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (TAMISEMI) Atajibu:-

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Mjimwema kimejengwa mwaka 2001. Kituo hiki kinaupungufu wa miundombinu ya jengo la Maabara, jengo la Mionzi, wodi za kulaza wagonjwa na wodi ya wazazi.

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Mjimwema ni miongoni mwa vituo vya afya Kongwe 358 vilivyofanyiwa tathmini ambavyo vinahitaji kufanyiwa ukarabati pamoja na kuongezewa miundombinu ya msingi ili viweze kutoa huduma stahiki ngazi ya Kituo cha Afya.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ukarabati wa vituo vya afya Kongwe kote Nchini ambapo jumla ya shilingi bilioni 164.86 zinahitajika. Aidha, katika mwaka wa fedha 2026/27 Serikali kupitia fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea imetenga shilingi milioni 31 kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la maabara katika Kituo cha afya Mjimwema.

UHITAJI WA KIDATO CHA TANO NA SITA SHULE YA SEKONDARI NGARA MJINI

MHESHIMIWA DOTTO JASSON BAHEMU (NGARA) Atauliza:-

Je, lini Serikali itaanzisha Kidato cha Tano na Sita katika Shule ya Sekondari Ngara Mjini.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (TAMISEMI) Atajibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikijenga shule mpya za kidato cha tano na sita au kuongeza miundombinu katika shule za sekondari zilizopo ili kuzipandisha hadhi kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na sita.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka wa fedha 2024/25 - 2025/26, Serikali imepeleka shilingi bilioni 2.08 katika halmashauri ya Ngara kwa ajili ya kuongeza miundombinu katika shule saba za sekondari za Rusumo, Kabanga, Lukole, Muyenzi, Murugamba, Ndomba na Ngara High School na kuzipandisha hadhi ambapo kwa sasa zina jumla ya wanafunzi 6,881 wa kidato cha tano na sita.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa shule ya Sekondari Ngara Mjini haina mahitaji makubwa ya kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na sita. Shule ya Sekondari Ngara Mjini ipo tarafa ya Nyamiaga yenye shule za tatu za Kidato cha Tano na Sita (Rusumo, Lukole na Ngara High) zenye jumla ya wanafunzi 2,915. Aidha, Serikali itaendelea kutenga fedha za ujenzi wa miundombinu ya kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na sita kwa kuzingatia tathmini ya mahitaji.

UJENZI WA SOKO LA KISASA HALMASHAURI YA MJI WA MBULU

MHESHIMIWA YUSTINA ARCADIUS RAHHI (VITI MAALUM) Atauliza:-

Je, lini Serikali itajenga Soko la Kisasa katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (TAMISEMI) Atajibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na soko la kisasa katika Mji wa Mbulu. Kwa kuzingatia umuhimu huo, mrati huu ni miongoni mwa miradi inayotarajiwa kutekelezwa kupitia mradi wa uoreshaji wa miundombinu ya Mji na Halmashauri nchini (TACTIC) awamu ya tatu.

Mheshimiwa Spika, Hatua zilizofiwa katika utekelezaji wa mradi huu ni pamoja na , Halmashauri ya Mji wa Mbulu kutenga eneo la ujenzi na taratibu zote za umiliki wa ardhi kwa ajili ya mradi huo. Aidha, tayari upembuzi yakinifu, usanifu wa kina wa majengo na gharama za mradi zimejulikana.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaanza ujenzi pindi taratibu za kibajeti zitakapo kamilika na Zabuni kutangazwa kuwapata wakandarasi na Washauri elekezi.

UJENZI WA BARABARA YA MUGOMBE-KAGERANKANDA

MHESHIMIWA EDIBILY KINYOMA KAZALA (KASULU VIJIJINI) Atauliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Barabara ya Mugombe-Kagerankanda,ambayo ni ahadi za Mheshimiwa Rais.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU-TAMISEMI Atajibu:-

Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2026/2027, Serikali imetenga kiasi cha shilingi Milioni 89.4 kwa ajili kufanya matengenezo ya kawaida na usanifu wa ujenzi wa barabara ya Mugombe-Kagerankanda kilomita 37 ili kupata gharama halisi za ujenzi wake ambapo baada ya kubaini gharama hizo, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza kazi hiyo. 

Mheshimiwa Spika, Aidha katika mwaka wa fedha 2025/2026 barabara hiyo ilifanyiwa matengenezo ya urefu wa kilomita 19 kwa kiwango cha changarawe kwa gharama ya Shilingi milioni 534.26. 

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuiboresha Barabara hii kwa tabaka la changarawe ili iweze kupitika misimu yote wakati maandalizi ya usanifu wa barabara hiyo yakiendelea. 

UKUZAJI WA SEKTA BINAFSI ILI KUONGEZA AJIRA

MHESHIMIWA DKT. REGINA CHRISTOPHER MALIMA (VITI MAALUM) Atauliza:-

Je, Serikali inajipangeje kuhakikisha inaimarisha mazingira ya uzalishaji na ukuaji wa sekta binafsi inayobeba ajira nyingi kwa vijana.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (MIPANGO NA UWEKEZAJI) Atajibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa sekta binafsi katika kuongeza uzalishaji, uwekezaji na ajira kwa vijana. Katika kutekeleza Dira 2050, Serikali imeandaa Mkakati wa Taifa wa Kuimarisha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI II), unaolenga kupunguza gharama za kufanya biashara, kurahisisha taratibu za uwekezaji na kuimarisha mazingira ya uzalishaji na utoaji wa huduma. Pia Serikali imesaini azimio la pamoja ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma la 2026.

Mheshimiwa Spika, Tathmini ya Utekelezaji wa MKUMBI I ya mwaka 2024, Tathmini ya Sekta Binafsi ya mwaka 2024 na Taarifa ya Hali ya Sekta Binafsi Tanzania ya mwaka 2026 zimebainisha mwenendo, changamoto na fursa za sekta binafsi nchini. Kwa kuzingatia matokeo na mapendekezo ya taarifa hizo, Serikali imeanza maandalizi ya kuandaa Sheria ya Maendeleo ya Sekta Binafsi, inayoleta kuimarisha uratibu wa taasisi za sekta binafsi, ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, pamoja na utawala bora ndani ya taasisi za sekta binafsi. Aidha, itaweka mfumo wa kushughulikia changamoto zinazoathiri uzalishaji, uwekezaji na ukuaji wa biashara kuanzia ngazi ya Kitaifa hadi mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, Serikali pia inaendelea kuimarisha majukwaa ya majadiliano na sekta binafsi pamoja na Idara za Viwanda, Biashara na Uwekezaji katika ngazi za mikoa na wilaya. Aidha, imeandaa Kipimo cha Ushindani wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (LGA Business and Investment Competitiveness Index) ili kuchochea utoaji huduma kwa wafanyabiashara na wawekezaji. Hatua hizi zinalenga kuongeza uzalishaji, ushindani wa biashara za ndani na uwekezaji unaopanua fursa za ujasiriamali na ajira zenye tija kwa vijana.

KUWEZESHA VIJANA NCHINI

MHESHIMIWA LATIFA KHAMIS JUWAKALI (VITI MAALUM) Atauliza:-

Je, Serikali haioni haja ya kuweka 4% au 10% kwa kila Wizara ya Kisekta kwa ajili ya kuwawezesha Vijana.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS – MAENDELEO YA VIJANA Atajibu:

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa uwezeshaji wa vijana ni jukumu mtambuka linalohitaji ushiriki wa Wizara zote za Kisekta kulingana na majukumu na fursa zilizopo katika sekta husika. Katika mwaka wa fedha 2025/26, Serikali kupitia Wizara mbalimbali imetumia kiasi cha Shilingi bilioni 966.8 kwa ajili ya programu na shughuli za uwezeshaji vijana, zilizowafikia vijana 6,933,835. Aidha, katika mwaka wa fedha 2026/27, Serikali imepanga kutumia takriban Shilingi trilioni 1.853 kwa ajili ya kuwawezesha vijana 18,644,433. Hatua hizi zinaonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kutenga rasilimali kwa ajili ya maendeleo na uwezeshaji vijana kupitia sekta mbalimbali. 

Mheshimiwa Spika, Serikali inapokea pendekezo la kutenga asilimia nne (4%) au kumi (10%) ya bajeti ya kila Wizara ya Kisekta kwa ajili ya uwezeshaji vijana, na italitathmini katika muktadha wa maandalizi ya mipango na bajeti za Serikali, kwa kuzingatia vipaumbele vya kitaifa, majukumu ya kisekta na upatikanaji wa rasilimali. Lengo ni kuhakikisha vijana wanapata fursa stahiki na kunufaika na programu za Serikali kwa kuzingatia vigezo na taratibu zilizowekwa. 

KUCHOCHEA MAPINDUZI YA KIDIjJITALI KATIKA SHUGHULI ZA KIUCHUMI NA KIJAMII

MHESHIMIWA ESTHER EDWIN MALLEKO (VITI MAALUM) Atauliza:-

Je, Serikali ina Mkakati gani katika kuchochea mapinduzi ya Kidijitali katika Shughuli za Kiuchumi na Kijamii.

WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI Atajibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea na utekelezaji wa Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali katika Tanzania ya Mwaka 2024 - 2034 (Tanzania Digital Economy Strategic Framework 2024 - 2034) unaoweka mwelekeo wa maendeleo ya Uchumi wa Kidijitali hapa Nchini.

Mheshimiwa Spika, Utekelezaji wa Mkakati huu unalenga kuongeza mchango wa Uchumi wa Kidijitali katika Pato la Taifa, kuimarisha tija na ufanisi katika shughuli za Kiuchumi na Kijamii, kupanua fursa za ajira na biashara, kuchochea ubunifu na uwekezaji pamoja na kuboresha ubora na upatikanaji wa huduma za Umma. Hatua hizi ni sehemu muhimu ya jitihada za Serikali za kujenga Jamii ya Kidijitali na zinaunga mkono utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

UJENZI WA BARABARA YA MTAMA – NEWALA

MHESHIMIWA YAHAYA ESMAIL NAWANDA (NEWALA VIJIJINI) Atauliza:-

Je, lini Barabara ya Mtama hadi Newala itajengwa kwa kiwango cha lami.

WAZIRI WA UJENZI Atajibu:-

Mheshimiwa Spika, Kazi za Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina wa barabara ya Mtama – Mkwiti – Newala yenye urefu wa kilometa 74 kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami zinaendelea na ziko katika hatua za mwisho. Baada ya kukamilika kwa hatua hii Serikali itatenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo. 


No comments