Filamu ya A Land Apart ya Nigeria Kuzindua Tamasha la ZIFF Goes Mainland 2026
Tamasha la
Kimataifa la Filamu la Zanzibar, ZIFF, kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya EU
pamoja na nchi wanachama wake 10 limezindua rasmi tamasha linalotembea la ZIFF
Goes Mainland EU MS Film Festival 2026.
Uzinduzi huo umefanyika leo Oktoba 19 2026
kupitia mkutano na wanahabari uliowakutanisha viongozi wa ZIFF na Mabalozi
pamoja na Wakuu wa Utumishi wa nchi washiriki katika kituo cha Alliance
Française jijini Dar es Salaam.
Viongozi na wawakilishi walioshiriki katika
uzinduzi huo ni pamoja na Balozi wa Umoja wa Ulaya Jean Marc Pisani Afisa
Mtendaji Mkuu wa ZIFF Alban Mwale Balozi wa Denmark Jesper Kammersgaard; Balozi
wa Ujerumani, Annett Günther; Balozi wa Italia, Joe Coppola;Mwambata wa
utamaduni wa ubalozi wa Ufaransa Ufaransa, Marie Escudier; Naibu ubalozi wa
Finland, Rosa Kotoaro; Naibu Ubalozi wa Hispania, Alba Espino Gómez; Kansela
Ubalozi wa Sweden, Lars Halvardsson; Mkuu wa Diplomasia ya Umma wa Ireland
Danai Lazaris pamoja na Afisa Uhusiano na Habari wa Poland, Magdalena Sękara
Kitundu.
Onyesho
rasmi la ufunguzi wa tamasha hilo litafanyika kesho Oktoba 20 saa 12 na nusu
jioni katika ukumbi wa Alliance Française jijini Dar es Salaam kwa kuonyeshwa
bure kwa filamu ya sayansi kutoka Nigeria inayojulikana kama A Land Apart
iliyonyakua Tuzo ya Dhahabu katika tamasha la ZIFF 2026.
Kazi hiyo inachanganya teknolojia ya Akili
Unde AI na maisha halisi ya Waafrika.
Balozi Pisani na Alban Mwale wamebainisha kuwa
msimu huu wa tano unaoongozwa na kaulimbiu Kuunganisha Mifumo Kutoka Mipaka ya
Kidijitali hadi ya Kibinadamu unalenga kuleta burudani ya kiwango cha juu huku
ukifungua milango ya majadiliano ya kiutamaduni kimazingira na mabadiliko ya
tabianchi kwa vijana kupitia filamu na usimulizi wa hadithi
Baada
ya ufunguzi jijini Dar es Salaam msafara huo wa wiki sita utazunguka katika
vyuo vikuu na vituo vya sanaa kwenye mikoa mitano ya Tanzania Bara kuanzia
Oktoba 20 hadi Desemba 2 2026.
Mkoani Pwani msafara utafika TASUBA Bagamoyo
Oktoba 27 na filamu ya Techplomacy kutoka Denmark, Mkoani Mwanza maonyesho
yatafanyika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine SAUT Oktoba 29 na 30 yakionyesha
filamu za Finding Connection kutoka Ujerumani, Prout iliyoratibiwa na programu
ya EU SASA Green and Smart Cities pamoja na Fantastic Machine; Novemba 16 maonyesho
yatarejea Dar es Salaam katika Chuo Kikuu cha Kampala na filamu ya Omen kutoka
Ubelgiji yakifuatiwa na kituo cha Ajabu Ajabu Novemba 17 na filamu ya Coconut
Head Generation kutoka Ufaransa; Chuo Kikuu cha Dar es Salaam UDSM kitakuwa
mwenyeji Novemba 18 na 19 na filamu za Fantastic Machine kutoka Sweden na Róise
na Frank kutoka Ireland huku Chuo cha Uandishi wa Habari DSJ kikipokea filamu
ya Je vida kutoka Finland Novemba 25
Mshindo
wa tamasha hilo utagonga pia mkoani Iringa katika Chuo Kikuu cha Ruaha Novemba
23 kupitia filamu ya Benvenuti in campagna Green Family kutoka Italia inayohusu
mazingira kabla ya kuhitimisha safari yake mkoani Dodoma katika Chuo Kikuu cha
UDOM Desemba mosi na mbili kwa maonyesho ya filamu za The Last Spark of Hope
kutoka Poland na La Caja 507 kutoka Hispania.
Baada ya kila onyesho mashabiki na wanafunzi
watapata fursa ya kushiriki majadiliano ya ana kwa ana na kupata elimu kuhusu
fursa za ufadhili wa masomo barani Ulaya kupitia programu ya Erasmus Plus huku
Balozi Pisani akisisitiza kuwa tasnia ya filamu ina uwezo wa kutengeneza ajira
kwa vijana katika uzalishaji ufundi na ujasiriamali wa kidijitali.
Post a Comment