MAKAMU WA RAIS ASHUHUDIA DAR CITY IKITWAA UBINGWA FAINALI YA KIKAPU

 


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, usiku wa Oktoba 18, 2026, ameshuhudia Timu ya Mpira wa Kikapu ya Dar City ikitwaa ubingwa wa Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) baada ya kuichapa Stein Warriors kwa vikapu 66 kwa 50 katika fainali iliyochezwa kwenye uwanja wa IST, Masaki.

 Fainali hiyo ilikuwa ya ushindani mkali tangu mwanzo, huku mashabiki waliojaa uwanjani wakizishangilia timu zao muda wote wa mchezo. James Amotre ameibuka nyota wa mchezo, akiisaidia timu yake kumaliza msimu ikiwa kileleni.

 Mara baada ya mchezo, Makamu wa Rais amekabidhi kombe la ubingwa kwa nahodha wa Timu ya Dar City, na kuzipongeza timu zote mbili kwa kiwango kizuri walichokionesha katika fainali hiyo.

 Amesema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya michezo na kuunga mkono maendeleo ya michezo nchini, ikiwemo mpira wa kikapu, ambao umeendelea kuvutia vijana wengi na kufungua fursa za ajira na kipato kupitia vipaji vyao.

 Makamu wa Rais, ametoa hamasa kwa wasanii pamoja na wafanyabiashara kudhamini timu za mpira wa kikapu ili kuwe na ushindani kama ilivyo katika mpira wa miguu hapa nchini. Aidha Makamu wa Rais amefurahishwa na ushiriki wa timu za wanawake katika ligi hiyo hali inayoashiria ukuaji wa mpira wa kikapu nchini. 










Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais, ameridhia kuwa mlezi wa mchezo wa mpira wa kikapu nchini kupitia ombi alilolitoa Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo Mhe. Paul Makonda.

 Mhe. Makonda amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuna miundombinu sahihi kwaajili ya michezo na burudani ikiwemo dhamira ya ujenzi wa Arena itakayotumika kwaajili ya shughuli za burudani na michezo. 

Fainali hizo zimehudhuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Patrobas Katambi, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, Waziri wa Kilimo Mhe. Daniel Chongolo, Naibu Waziri Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma (Mwana FA) Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Saad Mtambule, Wasanii, watu maarufu na wananchi mbalimbali wa Mkoa wa Dar es Salaam.

No comments