A LIST WAVUTANA 'LESO' YA FEDHA KATIKA MAPENZI
MJADALA kuhusu nafasi ya pesa katika mahusiano ya kimapenzi umeibuka tena, ukihusisha mastaa wa kipindi cha ‘A-List’ Irene Uwoya, Kajala Masanja na Aunty Ezekiel, baada ya kutofautiana mitazamo kuhusu majukumu ya mwanaume na mwanamke ndani ya uhusiano.
Akizungumza katika mazungumzo yao, Uwoya amesisitiza kuwa mwanaume anapaswa kuwa na pesa na kubeba sehemu kubwa ya majukumu katika mahusiano, akieleza anatakiwa kufanya takribani asilimia 90 ya mambo yanayohusu uhusiano huo.
Uwoya alisema mwanaume anatakiwa kujituma na kupambana kutafuta pesa, akiamini kuwa uwezo wa kifedha una nafasi kubwa katika kuimarisha mahusiano.
Kwa mtazamo wake, mapenzi bila pesa yanaweza kuwa magumu, huku akidai kuwa mwanamke anaweza kufikia hatua ya kuchoshwa na mwanaume ambaye hana uwezo wa kifedha.
Hata hivyo, kauli hiyo haikuonekana kukubalika kwa Aunty aliyeonesha kushangazwa na mtazamo wa Uwoya, akisisitiza kuwa majukumu ya kimahusiano hayapaswi kuachwa kwa mwanaume pekee.
Aunty ameeleza kuwa wenza wanapaswa kushirikiana katika kutimiza mahitaji na majukumu yao, badala ya kutegemea upande mmoja kufanya karibu kila kitu.
Aidha, ameonesha mashaka kuhusu upatikanaji wa wanaume wenye uwezo wa kutimiza matarajio yote ya kifedha yanayotajwa na Uwoya.
Tofauti hiyo ya mitazamo imeibua mjadala kuhusu nafasi ya pesa katika mapenzi na namna majukumu yanavyopaswa kugawanywa kati ya wapenzi.
Wakati Uwoya akisisitiza umuhimu wa mwanaume kuwa na uwezo wa kifedha na kubeba sehemu kubwa ya majukumu, Aunty anaamini kuwa ushirikiano wa pande zote mbili ni muhimu katika kujenga uhusiano.

Post a Comment