TCRA yazindua kampeni ya usalama mtandaoni
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA),Peter Mwasalyanda amesema mamlaka yake imezindua awamu mpya ya kampeni ya kuelimisha umma na taasisi kuhusu usalama mtandaoni.
Amesema kampeni hiyo inazingatia ulinzi wa data na namna ya kupunguza hatari ya binadamu katika ulimwengu wa kidijiti. Kampeni hiyo ya TCRA ni sehemu ya programu ya kimataifa ya uhamasishaji usalama mtandaoni inayotekelezwa mwezi wa Oktoba kila mwaka tangu 2004.
Tanzania ilijiunga na mpango huo wa dunia mwaka 2022 kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kwa ajili ya usalama na ufanisi wa huduma hiyo.
Aidha, Tanzania ni mojawapo ya zaidi ya nchi 200 zinazoadhimisha mwezi wa uhamasishaji kuhusu usalama wa mtandao na kampeni ya mwaka huu ikiwa na kaulimbiu ‘Usiwarahisishie Mambo’.
Kaulimbiu hii inaangazia umuhimu unaozidi kukua wa usalama wa mtandao katika maisha ya kila siku na inahimiza watu binafsi pamoja na wafanyabiashara kuchukua hatua muhimu za usalama wa mtandao ili kubaki salama wakiwa mtandaoni.
Mwasalyanda alisema: “Watumiaji wa mitandao wanahimizwa kutumia nywila imara, kutambua na kuripoti uhalifu wa mtandao. Wanapaswa pia kuthibitisha viungo visivyojulikana na jumbe ambazo hazijaombwa kabla hawajavifungua au kujibu”. Mwasalyanda alisema TCRA imeunda dirisha kwenye tovuti yake kwa ajili ya changamoto ya uelewa wa mtandao ili kupima viwango vya watumiaji vya uelewa wa usalama mtandaoni.

Post a Comment