Simba yachomoa yaitandika Yanga 2-1

 

Mchezo wa leo umeacha gumzo kubwa na furaha isiyo na kifani kwa mashabiki wa Simba baada ya kikosi hicho kufanikisha mpango wake wa kuvunja mwiko na kumaliza rasmi uteja uliokuwa ukiwasumbua mbele ya watani wao wa jadi Yanga.

Katika vita hiyo ya ya watani, ikiwa ni mechi ya mzunguko wa kwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara.kwenye Uwanja wa Uhuru mkoani Dar es Salaam, Simba iliibuka kidedea kwa mabao 2-1.

Kwa ushindi huo Simba inaongoza ligi ikiwa na pointi 21 na Yanga inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 18 baada ya zote kucheza michezo saba.Kuanzia msimu wa 2023/24 Simba ilifungwa na Yanga katika mechi zote za ligi kuu na katika msimu uliopita walitoka sare mechi zote mbili.

Katika pambano hilo lililokuwa na ushindani wa hali ya juu na presha kubwa tangu dakika ya kwanza, wachezaji wa Simba walionyesha nidhamu ya takriban kila eneo la uwanja, wakicheza kwa utulivu mkubwa, mbinu za hali ya juu na juhudi za pamoja zilizowafanya watawale mchezo na kuondoka na ushindi wa kihistoria.

Hata hivyo Yanga walianza kupata bao dakika ya tano lililofungwa na Peter Shalulile kwa kichwa akipokea pasi ya Maxi Nzengeli.

Baada ya bao hilo Simba walipambana kusawazisha na Yanga wakitafuta kulinda na kuongeza bao lingine lakini kipindi cha kwanza kilimalizika kwa Yanga kuwa mbele 1-0.

Kipindi cha pili mchezo ulianza kwa kasi Simba wakizidisha mashambulizi lakini walisubiri hadi dakika ya 68 kupata bao la kusawazisha kupitia Neo Mayema.







Baada ya bao hilo Simba waliongeza mashambulizi na dakika ya 71 Elie Mpanzu akaongeza bao la pili.

Matokeo haya yanamaanisha mwanzo wa zama mpya kwa Simba ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikipitia kipindi kigumu inapokutana na Yanga, huku safu yao ya usambazaji mpira na ushambuliaji ikionyesha makali ya tofauti na kuwafanya wapinzani wao kukosa majibu uwanjani.

 Ushindi huu sio tu kwamba umejaza pointi muhimu kwenye msimamo wa ligi na kuongeza morali kikosini, bali pia umerejesha heshima kubwa kwa klabu hiyo na kuwapa mashabiki wao sababu ya kutembea vifua mbele mtaani wakijivunia kiwango bora kilichoonyeshwa na timu yao.

Katika mchezo huo Simba walitawala kwa kumiliki mpira kwa asimilia 51 na Yanga 49 lakini wakiongoza kwa kucheza rafu 22 na Simba rafu 7 pekee.

No comments