KIWANDA CHA BURUDANI CHAPIGWA KUMBO LA MAANA: NETFLIX YAPUNGUZA WAFANYAKAZI 1,000 DUNIANI KOTE
Kipigo kikubwa kimepiga kiwanda cha burudani baada ya kampuni kubwa ya kurusha vipindi na filamu kwa njia ya mtandao duniani, Netflix, kutangaza kupunguza karibu asilimia 6 ya wafanyakazi wake wote, hatua inayowafuta kazi takribani watu 1,000 ikiwa ni idadi kubwa zaidi ya upunguzaji kazi katika kampuni hiyo ndani ya miaka minne iliyopita.
Idara zilizoathirika zaidi na mabadiliko haya ni pamoja na timu za usimamizi wa bidhaa, teknolojia, sheria pamoja na rasilimaliwatu (HR), ambapo hatua hiyo imekuja kufuatia kupungua kwa kasi ya ukuaji wa biashara ya kampuni hiyo na kuongezeka kwa ushindani mkubwa sokoni.
Wakurugenzi Wakuu Wenza wa Netflix, Ted Sarandos na Greg Peters, wametoa taarifa hiyo kupitia barua pepe maalum kwa wafanyakazi wote, wakieleza kuwa maamuzi hayo yamekuwa magumu lakini ni ya lazima ili kuwekeza rasilimali katika maeneo yenye tija zaidi na kuendeleza uvumbuzi.
Akiweka wazi changamoto hizo, Sarandos alisema kuwa ingawa biashara yao bado ni imara, ukuaji wake haujafikia kasi inayotakiwa, hali inayoshuhudiwa pia na anguko la hisa za kampuni hiyo kwa zaidi ya asilimia 40 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita huku thamani ya hisa ikishuka hadi chini ya dola 70 kutoka dola 125.
Mbali na changamoto za kiuchumi, Netflix imepitia kipindi kirefu bila kutoa mfululizo wa vipindi vipya vilivyoteka hisia za dunia kama ilivyokuwa kwa viwonyesho vya awali kama Stranger Things, Squid Game, au Wednesday, huku ushindani kutoka kwa wapinzani wao kama Apple TV na HBO ukiongezeka kwa kasi.
Ili kukabiliana na hali hiyo, Netflix imeanza kubadili mwelekeo wa biashara yake kwa kuwekeza zaidi kwenye matangazo ya moja kwa moja ya michezo kama vile mechi za Ligi ya Mpira wa Miguu Marekani (NFL) na pambano la ngumi la Tyson Fury dhidi ya Anthony Joshua, pamoja na kuingia kwenye usambazaji wa filamu kupitia majumba ya sinema kabla ya kuziweka mtandaoni.

Post a Comment