CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM CHAIDHINISHA MITAALA 494 NA KUONGEZA KASI YA MAGEUZI YA ELIMU



Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimepitia, kuandaa na kuidhinisha mitaala 494 hadi kufikia Juni mwaka huu, kiwango ambacho ni zaidi ya mara nane ya lengo la awali la mitaala 60, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ubora wa elimu na kuhakikisha programu zinazotolewa zinaendana na mahitaji ya soko la ajira.

Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye, ameyasema hayo wakati wa duru ya pili ya Mahafali ya 56 ya chuo hicho yaliyofanyika Mlimani Jijini Dar es Salaam, ambapo jumla ya wahitimu 2,774 wa shahada, stashahada na astashahada walitunukiwa vyeti vyao.

Profesa Anangisye ameeleza kuwa kati ya mitaala hiyo, mitaala 170 imekwisha pata ithibati kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), huku programu 47 zikianza kutolewa rasmi katika mwaka wa masomo 2025/2026, hatua inayofanikishwa kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) ambao pia umewezesha ujenzi na ukarabati wa majengo 21 chuoni hapo kufikia asilimia 93.

Katika kuimarisha ujuzi kwa vitendo na tafiti, UDSM imeingia ushirikiano wa kimkakati na sekta binafsi ikiwemo mkataba wa miaka mitatu na Kampuni ya PriceWaterhouseCoopers (PwC) Tanzania, mkataba wa miaka 10 na Kampuni ya Barrick Tanzania katika sekta ya madini, pamoja na ushirikiano wa miaka mitano na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Chuo cha Nelson Mandela katika matumizi ya Akili Unde (AI).

Mafanikio hayo yameendelea kujidhihirisha baada ya wataalamu 14 wa chuo hicho kutambuliwa na Wizara ya Elimu kwa kuchapisha tafiti kwenye majarida ya kimataifa, huku wanafunzi wake 89 kati ya 349 wakifanya vyema kwenye mitihani ya Bodi ya Wahasibu (NBAA) Mwezi Mei mwaka huu, pamoja na kuzinduliwa kwa karakana ya Shilingi bilioni 1.5 ya kubadilisha mifumo ya magari kutumia gesi asilia kwa kushirikiana na TPDC ili kuunga mkono nishati safi na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

No comments