NDEJEMBI AKIHITIMISHA MBIO ZA MWENGE ASISITIZA VITA DHIDI YA RUSHWA NA MIHADARATI
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratias John
Ndejembi, amehitimisha rasmi Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2026, huku akiwataka
Watanzania kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa, dawa za kulevya, maradhi na
umaskini, sambamba na kulinda amani, umoja na mshikamano wa kitaifa kama nguzo
muhimu za maendeleo.
Akizungumza katika Viwanja vya CCM Nelson Mandela, Sumbawanga mkoani
Rukwa, Makamu wa Rais amesema falsafa ya Mwenge wa Uhuru haipaswi kuishia
katika maadhimisho ya kuufunga, bali lazima itafsiriwe kwa vitendo kupitia
uwajibikaji, uzalendo na ushiriki wa wananchi katika kujenga Taifa lenye haki
na ustawi.
Amani na Mshikamano
Mhe. Ndejembi amesema Mwenge wa Uhuru ulioasisiwa na Baba wa Taifa,
Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, umeendelea kuwa alama ya ukombozi,
haki na mshikamano, akisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa utekelezaji wa
mipango mikubwa ya maendeleo, ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema kaulimbiu ya mwaka huu, “Tanzania ni yetu sote, tushikamane
kwa pamoja kuleta maendeleo,” inawakumbusha Watanzania wajibu wa kuweka
maslahi ya Taifa mbele ya tofauti za kisiasa, kidini na kimtazamo, huku
akisisitiza kuwa bila amani na utulivu hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana.
Mifumo ya Serikali
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amezitaka Wizara na Taasisi za
Serikali kutekeleza kwa vitendo agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la
kuhakikisha mifumo ya Serikali inasomana na kubadilishana taarifa ili
kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Ametolea mfano alichokishuhudia alipotembelea Maonesho ya Wiki ya Vijana
Kitaifa, ambapo Wizara mbili zinazoshughulikia masuala ya vijana—moja chini ya
Ofisi ya Waziri Mkuu na nyingine Ofisi ya Rais—zimebuni mifumo tofauti
inayolenga kuwahudumia vijana lakini mifumo hiyo haisomani, hali inayoweza
kuwaongezea usumbufu walengwa badala ya kuwarahisishia upatikanaji wa fursa.
Uondoaji Urasimu
Amesisitiza Wizara hizo kutekeleza maelekezo aliyoyatoa kwa Wenyeviti wa
Bodi na Taasisi za Serikali mkoani Arusha, Septemba 28, 2026, kwa kukaa pamoja
na kuandaa mpango wa kuwawezesha vijana kupata ujuzi kupitia mafunzo kwa
vitendo sehemu za kazi.
Sambamba na hayo, ametoa agizo la kuhakikisha mifumo iliyobuniwa
inaunganishwa ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa, huduma na fursa za
kiuchumi.
Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuondoa urasimu, kuongeza ufanisi wa
taasisi za umma na kuweka mazingira yatakayowawezesha vijana kunufaika na fursa
zilizopo, kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika uzalishaji mali.
Rushwa, Dawa za Kulevya
Akigeukia usimamizi wa miradi ya maendeleo, Makamu wa Rais amewataka
Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na watendaji wa Serikali kuhakikisha miradi
iliyokaguliwa, kuzinduliwa au kuwekewa mawe ya msingi na Mwenge wa Uhuru
inatekelezwa kwa ubora unaolingana na thamani ya fedha zilizotumika, huku hatua
stahiki zikichukuliwa dhidi ya uzembe na hujuma.
Aidha, amesisitiza kuimarishwa kwa mapambano dhidi ya rushwa, biashara
na matumizi ya dawa za kulevya, akibainisha kuwa vitendo hivyo vinadumaza
maendeleo na kuhatarisha nguvu kazi ya Taifa, hususan vijana.
Tahadhari
Kuhusu afya, Mhe. Ndejembi ameonya juu ya kuendelea kwa tishio la VVU na
UKIMWI, akibainisha kuwa takribani Watanzania milioni 1.7 wanaishi na VVU, huku
kiwango cha maambukizi kwa watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi kikiwa asilimia
4.4 kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2022/2023.
Amesema vijana, hususan wasichana na wanawake vijana, wanahitaji kupewa
kipaumbele katika elimu na huduma za kinga, sambamba na kuimarisha mapambano
dhidi ya malaria. Aidha, amewahimiza vijana zaidi ya milioni 21 nchini kutumia
fursa za kilimo, biashara, teknolojia na ujasiriamali ili kujenga uchumi wao na
kuchangia maendeleo ya Taifa.
Kumuenzi Mwalimu Nyerere
Akimkaribisha Makamu wa Rais kuhutubia wananchi, Waziri Mkuu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema maadhimisho ya
Mwenge wa Uhuru yanapaswa kuwa chachu ya Watanzania kuendeleza misingi ya Taifa
iliyoasisiwa na Baba wa Taifa, ikiwemo amani, umoja, upendo, haki, uzalendo,
uadilifu na utu.
Amesema misingi hiyo inapaswa kuongoza maisha ya kila siku na utendaji
wa viongozi, huku akibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan inaendelea kuimarisha misingi hiyo.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel
Nanauka, amesema Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2026 zimeendelea kuwa jukwaa
muhimu la kuhamasisha maendeleo, kuimarisha uzalendo na kuwashirikisha wananchi
katika kufuatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Ameongeza kuwa mbio hizi zimesaidia kutoa elimu ya mapambano dhidi ya
rushwa, dawa za kulevya na VVU/UKIMWI.
Wananchi Wataka Uwazi
Awali, akiwasilisha ripoti ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2026,
Kiongozi wa Mbio hizo Kitaifa, Wazo Mwang’onda, amesema wananchi wamepongeza
juhudi za Serikali katika kutekeleza miradi ya kimkakati.
Hata hivyo, amebainisha kuwa wananchi wameendelea kusisitiza umuhimu wa
kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za umma, pamoja
na kupanua fursa za uwezeshaji wa kiuchumi kwa vijana na wanawake kupitia
mikopo yenye masharti nafuu, mafunzo ya ujuzi na elimu ya ujasiriamali.
Mwang’onda amesema wananchi pia wamehimiza kuimarishwa kwa elimu ya uraia,
maadili na matumizi ya misingi ya sheria katika kushughulikia changamoto zao.
Mwenge wa Uhuru 2026
Makamu wa Rais, Mhe. Deogratias John Ndejembi, alikuwa mgeni rasmi
katika kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2026, akimwakilisha Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Maadhimisho hayo yaliyofanyika Sumbawanga mkoani Rukwa yameenda sambamba
na kumbukizi ya miaka 27 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere, pamoja na Maonesho ya 26 ya Wiki ya Vijana Kitaifa, huku yakihitimisha
safari ya Mwenge wa Uhuru iliyoanza Aprili 2, 2026.
mwish









Post a Comment