KUKUTANA KWA DKT MWIGULU NCHEMBA NA DIASPORA KWADHIHIRISHA NIA YA AWAMU YA SITA KUSHIRIKISHA WATANZANIA WOTE KATIKA MAENDELEO YA TAIFA

 



 

WATANZANIA waishio ughaibuni wamesema tukio la Tanzania Diaspora Business Forum 2026 lililofanyika jijini London limeendeleza kwa vitendo dhana ya kuwathamini wazalendo wanaoishi nje na kuwajumuisha kikamilifu katika kuchangia maendeleo ya kiuchumi nchini Tanzania.

Hatua ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuwafuata na kukutana ana kwa ana na Watanzania hawa ughaibuni inadhihirisha nia thabiti ya kutambua mchango wao mkubwa kama wadau muhimu wa maendeleo ya Taifa.

Mmoja wa watanzania aishie Uingereza Freddy Macha amesema kwamba mkutano huo uliokuwa na lengo la kuunganisha juhudi za Watanzania walioko nyumbani na walioko nje ya nchi, ulifana na kuonesha nia ya serikali kwa wanadiaspora ya kuwataka kuwekeza mitaji na ujuzi wao katika miradi mbalimbali ya kimkakati nchini Tanzania.

Macha alisema katika andiko lake kwamba, mamia ya Watanzania walisafiri kutoka majimbo na maeneo mbalimbali ikiwemo Uingereza, Scotland, Ireland na Wales ili kukutana na Waziri Mkuu Dkt Mwigulu Lameck Nchemba katika hoteli za Marble Arch na Millennium Gloucester Kensington.

Mkutano huo uliwajumuisha zaidi ya wajumbe mia tatu na hamsini kutoka vikundi na taasisi mbalimbali kama TZ UK, ATUK, Zanzibar Welfare Association in the UK na Tanzania UK Business Group, ulifanyika katika mazingira rafiki.

Waziri Mkuu Dkt Nchemba ambaye aliambatana na ujumbe mzito wa viongozi na watendaji wa Serikali akiwemo Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Angella Kairuki, Balozi wa Tanzania Uingereza Mbelwa Kairuki, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje Balozi Said Shaib Mussa, Makatibu Wakuu wa Mipango, Uwekezaji na Uchumi wa Bluu, pamoja na Watendaji Wakuu wa TISEZA na ZIPA,alieleza kwa kina hatua kubwa ambazo Serikali imezichukua katika kukuza uchumi na kuboresha miundombinu ili kuweka mazingira salama na yenye tija kwa uwekezaji wao.

Akiwahutubia wanadiaspora hao, Dkt Mwigulu Alibainisha kuwa uchumi wa nchi umeendelea kuimarika licha ya kukabiliwa na changamoto za kimataifa na kitaifa kama athari za UVIKO 19, mabadiliko ya sera za biashara duniani, migogoro ya kivita Mashariki ya Kati, uhaba wa fedha za kigeni na maafa ya mafuriko Hanang.

Katika sekta ya usafirishaji, alieleza kukamilika kwa ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma, maendeleo ya vipande vya Isaka hadi Mwanza, Tabora na Manyoni ili kuunganisha na Makutupora, na matarajio ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuzindua rasmi reli ya Dar es Salaam hadi Mwanza kabla ya kumalizika kwa awamu yake ya pili.

Akiendelea kufafanua fursa hizo za kiuchumi, Waziri Mkuu alieleza kuhusu maendeleo ya upembuzi yakinifu wa reli ya kimataifa ya kutoka Uvinza na Kigoma kwenda Musongati na Gitenga Burundi mpaka Kindu na Uvira DRC, ambayo pindi itakapokamilika itakuwa ya kwanza kwa urefu barani Afrika na ya tano duniani.

Pia aligusia mchakato wa kumpata mkandarasi wa reli ya Mtwara hadi Mbamba Bay pamoja na utekelezaji wa miradi ya bomba la mafuta. Katika sekta ya nishati na maji, alieleza kuwa umeme umeunganishwa katika vijiji vyote nchini na sasa juhudi zipo kwenye vitongoji na nishati safi ya kupikia, huku vijiji visivyo na maji vikiwa vimepungua hadi chini ya elfu moja. Kwenye elimu, alitangaza maandalizi ya elimu ya lazima hadi kidato cha nne kuanzia Januari 2028 itakayopokea wanafunzi zaidi ya milioni tatu, ikihusisha ujenzi wa madarasa elfu kumi na sita na maabara elfu hamsini.





Katika sekta ya afya, Serikali imesogeza huduma bora karibu na wananchi kwa kuboresha miundombinu na kuweka vifaa tiba vya kisasa kama MRI, CT Scan na Ultrasound hadi ngazi ya hospitali za wilaya. Dkt Mwigulu alihitimisha kwa kueleza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kipato cha kati cha juu, akisisitiza kuwa Serikali inaweka mazingira wezeshi na inawahitaji Watanzania wote wa nyumbani na walioko ughaibuni kushirikiana na kuwekeza katika sekta zenye fursa kubwa kama vile madini, kilimo, mifugo, uvuvi, utalii na uchumi wa bluu.

Kama sehemu ya utekelezaji wa vitendo wa kuondoa vikwazo na kuingiza wanadiaspora katika mfumo wa kiuchumi, mikutano hiyo ilihusisha vikao vidogo vya kibiashara, ushirikishwaji wa mabenki makubwa ya nyumbani kama CRDB, NMB na Azania, pamoja na makampuni ya uwekezaji wa majengo kama Hamidu City Park.

Pia wanadiaspora walipata fursa ya kukutana na mmiliki wa kampuni ya NALA Benjamin Fernandes inayoshughulikia usafirishaji wa fedha, huku wakitatuliwa changamoto zao za kisheria na uraia kupitia huduma za usajili wa Vitambulisho vya Taifa zilizotolewa papo hapo na Maafisa wa NIDA waliosafirishwa kutoka Tanzania wakiongozwa na Maryamu Issa, wakisaidiwa na Afisa Uhamiaji wa Ubalozi Ally Mtanda.

Ili kuhakikisha sauti na kero zao zinazungumzwa na kufanyiwa kazi kwa haraka, wanadiaspora walikabidhiwa namba ya simu ya WhatsApp ya Waziri Mkuu kwa ajili ya mawasiliano ya moja kwa moja.

 

No comments