MAVUNDE AHIMIZA NCHI ZA AFRIKA KUTUMIA MADINI KUKUZA VIWANDA NA AJIRA
Waziri wa Madini wa Tanzania, Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde, amezitaka nchi za Afrika kuacha kufanya kazi kwa kujitenga kwa kuunganisha nguvu katika usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za madini ili kukuza viwanda, kutengeneza ajira, na kuimarisha uchumi wa bara hilo.
Wito huo ulitolewa Oktoba 19, 2026 jijini Accra, Ghana, wakati akizungumza katika mjadala wa jopo la Mawaziri kutoka Tanzania, Nigeria, na Liberia uliokuwa na mada kuhusu kuzitafsiri dira za madini kuwa vitendo katika Mkutano wa Kimataifa wa Mining in Motion unaofanyika kuanzia tarehe 19 hadi 21 Oktoba 2026.
Waziri Mavunde alisisitiza kuwa wakati umefika kwa nchi za Afrika kuweka pembeni tofauti zao na kushirikiana kikamilifu katika kutekeleza mikakati ya pamoja ya maendeleo ya sekta ya madini.
Katika mchango wake, Waziri Mavunde alibainisha kuwa ingawa bara la Afrika linamiliki zaidi ya asilimia 32 ya rasilimali za madini muhimu zinazojulikana duniani, sehemu kubwa ya utajiri huo bado inasafirishwa nje ya bara bila kuongezwa thamani ya kutosha.
Hali hiyo alisema imekuwa ikizinyima nchi za Afrika fursa muhimu za kujenga viwanda vya ndani, kutengeneza nafasi za kazi kwa vijana, na kuongeza mapato ya Serikali. Alisisitiza kuwa Dira ya Madini ya Afrika haipaswi kubaki kama nyaraka na majadiliano ya mezani tu, bali inapaswa kuambatana na utekelezaji wa vitendo kupitia mifumo thabiti ya mazungumzo na maamuzi ya pamoja ili kuharakisha ufikiaji wa malengo yaliyowekwa.
Akieleza mafanikio na hatua ambazo Tanzania imepiga, Waziri Mavunde alieleza kuwa mageuzi ya kisheria yaliyofanyika mwaka 2017 yameimarisha usimamizi wa rasilimali na ushiriki wa Serikali, huku hatua za kuzuia usafirishaji wa madini ghafi zikichochea uongezaji thamani nchini.
Chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania hivi sasa ina zaidi ya viwanda vinane vya kusafisha dhahabu na viwanda zaidi ya 16 vya uchakataji na usafishaji wa madini ya metali za msingi. Hatua hizi zimeifanya sekta ya madini kuchangia asilimia 10.3 ya Pato la Taifa, huku wachimbaji wadogo wakichangia takribani asilimia 40 ya uzalishaji wote wa sekta hiyo kutokana na uwezeshaji wa dhati wa Serikali.
Katika eneo la ushirikiano wa kikanda, Waziri Mavunde alitaja nchi za Tanzania, Madagascar, na Msumbiji kuwa na fursa ya kipekee ya kuunganisha nguvu katika uendelezaji na uchakataji wa madini kinywe (graphite) pamoja na kuoanisha sera ili kujenga mnyororo wa thamani unaowanufaisha wananchi wa mataifa hayo.
Alitoa wito kwa viongozi na wadau wa Afrika kubadili mtazamo na kugeuza utajiri wa madini kuwa fursa za viwanda, ajira, na teknolojia, badala ya kuendelea kuuza madini ghafi na kisha kununua bidhaa zilizosindikwa kutoka nje ya bara kwa gharama kubwa.
Akifungua rasmi mkutano huo, Rais wa Jamhuri ya Ghana, Mheshimiwa John Dramani Mahama, alisema kuwa ni wakati muafaka kwa Afrika kuelekeza nguvu kwenye soko la madini muhimu na ya kimkakati kutokana na ongezeko la mahitaji ya nishati safi duniani.
Rais Mahama alisisitiza kuwa lengo kuu linapaswa kuwa kuyaongezea thamani madini hayo ndani ya bara la Afrika kabla hayajasafirishwa kuelekea katika masoko ya dunia, ili kuhakikisha faida kubwa inabaki kwa wananchi wa Afrika.
Post a Comment