Kiongozi wa Dini Ahimiza Amani na Subira Tunduru Huku Serikali Ikitakiwa Kuchukua Hatua za Kisheria Kupunguza Mizozo
Shehe Abdulmanafi Hassan Chikagula ametoa wito mzito kwa wananchi wa kata ya Misechela, tarafa ya Namasakata wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, kudumisha amani na kuepuka kulipiza kisasi kufuatia mizozo na migogoro iliyotokea.
Akizungumza wakati wa kutoa mawaidha kwenye maziko ya aliyekuwa Diwani wa Kata ya Misechela, Zubery Abbas Binamu, pamoja na raia wenzake waliopoteza maisha, Shekhe Chikagula aliwataka wananchi kutoingia kwenye mkumbo wa vurugu na badala yake kuiamini serikali na vyombo vya dola katika kuchukua hatua za kisheria ili kurejesha utulivu na kuwapata waliovunja sheria kwa kufuata taratibu.
Kiongozi huyo wa dini alieleza masikitiko yake kuhusu mazingira yaliyochangia kuvunjika kwa amani na kuwataka viongozi wa maeneo hayo kuwa waadilifu.
Aliitaka serikali kuimarisha ulinzi, hasa katika maeneo ya pembezoni mwa mipaka, ili kuwahakikishia wananchi usalama wa maisha yao na mali zao, huku akisisitiza kuwa utatuzi wa changamoto za rushwa na matumizi mabaya ya madaraka utasaidia kurudisha nidhamu, usawa na amani endelevu kati ya wakulima na wafugaji.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Abdalah Mmala, alisema kuwa wilaya imepata mshtuko mkubwa kutokana na vifo hivyo, akibainisha kuwa marehemu Diwani Binamu alikuwa kiungo muhimu sana kati ya halmashauri na wananchi katika kuleta maendeleo na amani.
Pia, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini, Ado Shaibu, alitoa pole kwa familia na kusisitiza umuhimu wa kurejesha utamaduni wa kuishi kwa amani na utulivu, huku akiahidi kushirikiana na mbunge wa Tunduru Kusini kusimamia haki za wananchi na kuitaka serikali kutekeleza sheria na taratibu za matumizi ya ardhi ili kumaliza mizozo hiyo mara moja.
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Denis Masanja, alieleza masikitiko yake makubwa kwa kupoteza maisha ya viongozi na wananchi, akisisitiza kuwa serikali haitavumilia vitendo vyovyote vinavyotia doa amani ya wilaya hiyo. Aliahidi kuwa vyombo vya dola vitaendesha operesheni maalum na kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya watu wote waliohusika na uvunjifu wa amani, ili kuhakikisha usalama unarejea kikamilifu.
Akithibitisha kuwapo kwa matukio hayo na majeruhi waliopata matibabu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya, alieleza kuwa jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi na operesheni kabambe ya kuwasaka wote waliohusika. Alibainisha kuwa tayari watuhumiwa 15 wamekamatwa ili kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, hatua inayolenga kurejesha utulivu, haki na amani kwa jamii nzima ya Tunduru.





Post a Comment