Waziri Masauni Akagua Maeneo Yaliyoathirika na Mafuriko Kigoma Ujiji
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Hamad Yusuf Masauni, amefanya ziara katika maeneo yaliyoathirika na mafuriko katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, mkoani Kigoma, kwa lengo la kujionea hali halisi na kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto hiyo kabla ya kuanza kwa mvua za El Niño zinazotarajiwa.
Katika ziara hiyo iliyofanyika Oktoba 17, 2026, Waziri Masauni alitembelea eneo la Kibirizi na kukagua athari za mafuriko pamoja na uharibifu wa mazingira, kabla ya kuelekea Katubuka, eneo ambalo pia linakabiliwa na changamoto kubwa ya mafuriko.
Akiwa Katubuka, Mhe. Masauni amewapa pole wananchi walioathirika na mafuriko hayo, huku akiahidi kuwa Serikali itafanyia kazi changamoto zinazowakabili kwa kuzingatia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, amewapongeza wananchi kwa kuendelea kuwa wavumilivu wakati Serikali ikiendelea kutekeleza wajibu wake wa kutafuta suluhisho la kudumu.
Waziri Masauni amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari, ikiwemo kutafuta maeneo salama ya kuishi inapohitajika, hususan katika kipindi hiki cha maandalizi ya mvua za El Niño. Vilevile, amewahimiza kushirikiana na viongozi wa maeneo yao ili kurahisisha utekelezaji wa hatua zinazochukuliwa na Serikali.
Katika hatua nyingine, Mhe. Masauni alikagua ujenzi wa mtaro unaolenga kupitisha maji kutoka eneo la Katubuka na kuyaelekeza ziwani, ikiwa ni moja ya hatua za haraka za kupunguza athari za mafuriko katika eneo hilo.
Akitilia mkazo dhamira ya Serikali, Waziri Masauni amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuchukua hatua za vitendo. “Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan si Serikali ya mchakato na maneno, bali ni Serikali ya vitendo,” alisema Mhe. Masauni.
Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kufuatilia changamoto za mafuriko na uharibifu wa mazingira, pamoja na kuimarisha hatua za tahadhari na utatuzi ili kulinda maisha ya wananchi na mali zao.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Mhe. Dkt. Rashid Chuachua, alieleza kuwa kuanzia mwaka 2023 hadi 2025 Manispaa ya Kigoma Ujiji ilipata mvua zilizokuwa juu ya wastani na kusababisha athari mbalimbali.
Alibainisha kuwa kata zilizoathirika kwa kiwango kikubwa ni pamoja na Katubuka, Kibirizi, Bangwe na Buzebazeba, ambapo maji yaliingia kwenye nyumba zilizopo jirani na Bwawa la Katubuka. Aliongeza kuwa Halmashauri ya Manispaa inaendelea kuchukua hatua mbalimbali, ikiwemo kutoa elimu kwa wakazi wa maeneo hayo na maeneo mengine hatarishi.

Post a Comment