TANZANIA KUTUMIA FURSA ZA MIKUTANO YA IMF NA BENKI YA DUNIA, BANGKOK-THAILAND KIMKAKATI
Waziri
wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ameongoza kikao cha maandalizi ya
Ushiriki wa Ujumbe wa Tanzania katika Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la
Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (World Bank Group), inayofanyika jijini
Bangkok nchini Thailand, kuanzia tarehe 12 hadi 18 Oktoba 2026, huku
akisisitiza kuwa Tanzania imejipanga kikamilifu kunufaika na mikutano hiyo
kiuchumi na kijamii.
Mhe. Balozi Omar amebainisha kuwa ushiriki wa Tanzania ni wa
kimkakati kwa ajili ya uhamasishaji wa rasilimali na usimamizi wa fedha za nje
nchini, kama mwanachama wa taasisi hizi, na kutumia fursa hiyo kufanya
mazungumzo ya ngazi ya juu na viongozi wa taasisi hizo, ikiwemo Makamu wa Rais
anayesimamia Kanda ya Kusini Mashariki mwa Afrika na wakurugenzi watendaji, ili
kuendeleza ajenda za maendeleo.
“Moja ya maeneo muhimu yanayopewa kipaumbele ni utekelezaji
wa mzunguko wa 21 wa IDA (IDA 21), ambayo Serikali imewasilisha orodha ya awali
ya miradi inayotarajiwa kufadhiliwa na Benki ya Dunia na kuhakikisha kuwa miradi
ya kipaumbele ya Taifa inapata ufadhili unaostahili” alisema Mhe. Balozi Omar.
Mbali na Benki ya Dunia, Tanzania inapanua wigo wa
ushirikiano na wadau wengine wa maendeleo na inaendelea na mazungumzo na
mashirika ya ukadiriaji wa mikopo kama Moody's na Fitch, pamoja na kuvutia
wakopeshaji wapya ili kuongeza fursa za upatikanaji wa fedha na kuimarisha
imani ya wawekezaji kwa uchumi wa Tanzania.
Kwa
ujumla, Serikali imesisitiza kuwa ushiriki wake katika mikutano hii si tu wa
kuimarisha kidiplomasia ya kiuchumi, bali ni wa kiutendaji ili kuhakikisha kuwa
kila fursa ya ufadhili inatumika ipasavyo, miradi inatekelezwa kwa viwango
vinavyokubalika, na pale inapobidi, serikali itatafuta msaada wa kibajeti (GBS)
ili kukidhi mahitaji ya rasilimali katika programu mbalimbali za maendeleo.
Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa Majukumu ya Ubalozi
wa Heshima nchini Thailand, Balozi wa Heshima wa Tanzania nchini humo Mhe.
Florean Rwehumbiza, alieleza kuwa Ofisi yake inaendelea kuimarisha ushirikiano
wa diplomasia ya kiuchumi kupitia uhusiano wa kibiashara, utalii, na huduma za
afya kati ya nchi hizo mbili.
Alibainisha kuwa Ofisi yake imekuwa ikifanya kazi kubwa ya
kutangaza utalii wa Tanzania katika nchi za Kusini-Mashariki mwa Asia, ikiwemo
Malaysia, Vietnam, Cambodia, Lao, na Hong Kong, jitihada ambazo zimezaa matunda
kwa kushawishi mashirika ya ndege kuanza safari za moja kwa moja kuelekea
Tanzania, jambo linalolenga kurahisisha usafiri kwa watalii na wafanyabiashara.
Kuhusu sekta ya afya, Mhe. Rwehumbiza alisema kuwa Tanzania
imekuwa nchi ya pili barani Afrika kwa kupeleka wagonjwa nchini Thailand kwa
ajili ya matibabu ambapo Takwimu zinaonesha kuwa kuanzia Desemba mwaka jana
hadi Juni mwaka huu, Watanzania wametumia taktiban pesa za Thailand (Thai Baht)
milioni 150 kwa huduma za matibabu nchini humo.
Katika upande wa usafiri, alisisitiza kuwa Tanzania ndiyo
nchi pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki inayoruhusiwa kuingia Thailand
bila kuhitaji kadi ya homa ya manjano (yellow fever card), mradi msafiri
asipitie Nairobi, Aidha, ofisi hiyo inaendelea kupigania upatikanaji wa mfumo
wa visa on arrival kwa wasafiri kutoka Tanzania ili kurahisisha zaidi
mwingiliano wa watu.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kidumu ya Bunge ya
Bajeti, Mhe. Ali Hassan Omar, aliipongeza Wizara ya Fedha kwa kulishirikisha
Bunge katika Vikao hivyo vya Mwaka vya IMF na Benki ya Dunia na namna Serikali
inavyofanya jitihada za kuhakikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050
inatekelezwa kwa mafanikio kupitia upatikanaji wa rasilimali ferha na mipango
mbalimbali ya kukuza uchumi.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Waziri wa Fedha-Zanzibar,
Mhe. Dkt. Juma Malik Akil (Mb), Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti
ya Bunge, Mhe. Ali Hassan Omar (Mb), Mjumbe wa Kamati ya Bajeti ya Bunge, Mhe.
Enock Zadock Koola (Mb), Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa
Serikali, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango, ambaye
pia ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Kida, Gavana wa
Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba na Viongozi wengine waandamizi wa
Serikali na baadhi ya Taasisi zake.

Post a Comment