Jiji la Dar es Salaam Laagizwa Kuboresha Usimamizi wa Dampo la Pugu na Utunzaji wa Mazingira




Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imeelekeza uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuwa na mpango madhubuti wa kusimamia dampo la Pugu Kinyamwezi, ili kudhibiti na kukabiliana na athari za kiafya na kimazingira.

Kamati hiyo imesisitiza usimamizi madhubuti wa Sheria ya Mazingira, huku ikishauri kupanuliwa kwa wigo wa ujenzi wa madampo mapya katika maeneo mengine kulingana na mahitaji, hatua itakayosaidia kupunguza changamoto ya uzagaaji wa taka.

Maelekezo hayo yametolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Prof. Pius Yanda, pamoja na baadhi ya wajumbe wakati wa ziara ya kukagua hali ya mazingira katika eneo hilo mwishoni mwa wiki. 

Ziara hiyo ililenga kufuatilia utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, mnamo Septemba 18, 2026, kuhusu kuboresha usimamizi wa taka katika dampo hilo.

Mhe. Prof. Yanda, ambaye pia ni Mbunge wa Buhigwe, alieleza kuwa ni muhimu afya za wananchi wanaoishi kando ya dampo hilo zikapewa kipaumbele kwa kuchukua hatua stahiki, ikiwemo ujenzi wa uzio kulizunguka.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wabunge walitaka kufanyike ufuatiliaji wa kina ili kubaini athari za kiafya zinazowapata wakazi hao kutokana na moshi na harufu mbaya ya mrundikano wa taka, kisha hatua za haraka zichukuliwe. Walisisitiza uwepo wa wazabuni wa ukusanyaji wa taka wenye vifaa na uwezo wa kufanya kazi hiyo kwa ufanisi, ili kuhakikisha miji inakuwa safi na ya kuvutia, hususan Dar es Salaam ambacho ni kioo cha nchi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Reuben Kwagilwa, aliyeambatana na wataalamu katika ziara hiyo, alisema Serikali itaendelea kuhakikisha suala la usafi wa mazingira linafanyika inavyopaswa. Alieleza kuwa msimamo wa Serikali ni kuhamasisha wadau kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa taka kwa kuzigeuza kuwa fursa za kiuchumi.

Halikadhalika, Mhe. Kwagilwa alitaka apatikane mwekezaji imara wa kusimamia uchakataji wa taka katika Dampo la Pugu ili kupunguza athari za afya na mazingira kwa jamii inayolizunguka. Pia aliielekeza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kushirikiana kwa karibu na taasisi zote za mazingira, likiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ili kuhakikisha mradi huo unakuwa endelevu.

Katika hatua nyingine, Kamati hiyo ilitembelea eneo la Mto Ng'ombe wilayani Kinondoni na kupongeza jitihada zinazofanyika za kuboresha mazingira ya mito mbalimbali mkoani humo.

Mhe. Prof. Yanda alisema maboresho yaliyofanyika, ikiwemo ujenzi wa kingo za mito, yamekuja wakati muafaka. Alipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa usimamizi mzuri wa mazingira unaojenga ustawi wa afya ya jamii na kusisitiza umuhimu wa kuongeza wigo wa upanuzi wa mito mingine ili wananchi wengi zaidi wafaidike.

No comments