JUMUIYA ZA KIRAIA ZAASWA AMANI, UMOJA NA MSHIKAMANO WA TAIFA




RAIS Dk Samia Suluhu Hassan ameagiza jumuiya za kiraia zitekeleze wajibu wao kikatiba, ikiwemo kulinda amani na kujenga umoja na mshikamano wa taifa. Dk Samia aliagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhakikisha changamoto za jumuiya za kiraia zinachakatwa, kutatuliwa na kugeuzwa kuwa fursa ya kudumisha utulivu wan chi. 

Alisema hayo kupitia hotuba yake iliyosomwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi alipomwakilisha katika kufungua maadhimisho ya miaka 70 ya usajili wa jumuiya za kiraia Dar es Salaam jana. 

Dk Samia alisema kwa kuwa jumuiya za kiraia ni sehemu ya maisha ya Watanzania, zina dhima muhimu kujenga na kuimarisha mshikamano wa kitaifa. 

“Kujenga umoja wa kitaifa sio jukumu la serikali pekee, bali ni jukumu la kila Mtanzania zikiwemo jumuiya zote za kiraia nchini,” alisema Dk Samia. 

Aliongeza kuwa pamoja na tofauti za kiimani zilizopo miongoni mwa Watanzania, jumuiya za kiraia zinapaswa kuwa wamoja ili kuwajenga Watanzania katika mshikamano.

 “Ili kujenga mshikamano imara wa kitaifa, lazima Watanzania wajenge utamaduni wa kuvumiliana kufikia maendeleo yanayotarajiwa na huo ndio msingi mkuu wa maendeleo ya nchi,” aliongeza Dk Samia. 

Alisema kuyafikia hayo yote, utashi na umoja wa kitaifa lazima utokane na wananchi wenyewe. Sambamba na hayo, alisema jumuiya za kiraia zimekuwa wadau wakweli wa maendeleo kutokana na uwekezaji wao katika sekta mbalimbali hapa nchini. 

Dk Samia alizitaka jumuiya za kiraia kuendelea kuweka maslahi ya nchi mbele, huku zikitafuta suluhu ya migogoro pamoja na kutengeneza utaratibu utakaozuia migogoro isitokee. 

Alizitaka pia wizara zote kutoa ushirikiano wa dhati kwa jumuiya hizo ili iwe rahisi kutekeleza majukumu yao ya kutoa huduma kwa Watanzania. 

“Hivi karibuni kumetokea matishio ya mmomonyoko wa maadili nchini kwetu, jumuiya za kiraia zinawajibika katika kulinda maadili ya kitaifa na kujenga ustawi wa kila Mtanzania,” alisisitiza Dk Samia. 

Aidha, Dk Samia alisema asilimia kubwa ya Watanzania wanapatikana katika jumuiya za kiraia, hivyo watumie jumuiya hizo kuliponya taifa na kwamba kama kuna tatizo, zitumike njia za hekima na busara kuishauri serikali namna bora ya utatuzi wake.

 “Jumuiya za kiraia zipo huru katika kutekeleza wajibu wake, hivyo tumieni uhuru huo katika kuleta usalama, amani, umoja na mshikamano kwa Watanzania,” aliongeza Dk Samia. 

Aliahidi serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa jumuiya za kiraia ili kuwafanya Watanzania wote waweze kufaidika na kazi nzuri za jumuiya na taasisi hizo. Dk Samia aliitaka pia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Msajili wa Jumuiya za Kiraia kuandaa matamasha yenye lengo la kuhamasisha amani, huku zikiongeza ufanisi na tija katika kuwahudumia Watanzania.

 Kwa upande wake, Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa alizitaka jumuiya zote zilizosajiliwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria ili kuondoa migongano na serikali. 

Alisema serikali ina wajibu wa kufuatilia na kujiridhisha na mienendo ya jumuiya zilizosajiliwa kama zinatekeleza majukumu yaliyoainishwa katika katiba zao.

 Kihampa aliongeza kuwa serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ina wajibu wa kusaidia jumuiya za kiraia katika utekelezaji wa majukumu yake. 

Alisema jumuiya hizo nazo zina wajibu wa kutoa elimu kupitia matamasha yenye lengo la kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza amani na utulivu wa nchi. Vilevile, alisema serikali ina wajibu wa kuzileta pamoja jumuiya za kiraia na kujadili namna bora ya kuepuka kufanya makosa katika utekelezaji wa kazi zao na kwamba hadi sasa kuna jumuiya 12,000 zilizosajiliwa Tanzania Bara.

No comments