KAMATI YA BUNGE YATAKA UHAKIKI WA LAINI ZA SIMU
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeishauri serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na kampuni za simu kuhakiki wamiliki wa laini za simu ili kudhibiti uhalifu wa mtandaoni.
Ilishauri pia serikali kuweka utaratibu wa kusajili laini za simu katika maduka ya kampuni husika na kuboresha mifumo ya kubaini matumizi yasiyo ya kawaida pamoja na kurahisisha utoaji wa taarifa na kufungiwa kwa laini zinazotumika kutekeleza uhalifu wa mtandaoni.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mashimba Ndaki alisema licha ya mafanikio yaliyopatikana katika matumizi ya laini za simu za kiganjani, changamoto za kiusalama bado zinaongezeka.
Ndaki alisema hayo wakati akiwasilisha mapendekezo ya kamati hiyo kuhusu mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka wa Fedha 2027/2028 na mapitio ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali katika kipindi cha muda wa kati.
Alisema mwaka 2025 laini za simu za kiganjani ziliongezeka hadi 106,823,601 kutoka 86,769,161 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 23.1. Ndaki alisema pia laini za simu za mezani ziliongezeka kwa asilimia 42.5, kutoka 78,299 mwaka 2024 hadi 111,600 mwaka 2025.
Alisema kamati hiyo imebaini kuwepo kwa changamoto za usajili wa laini kwa kutumia vitambulisho vya watu wengine, kuongezeka kwa uhalifu wa mtandaoni na kuchelewa kwa mamlaka husika kuchukua hatua dhidi ya namba zinazotumika katika uhalifu huo, ikiwamo kuzifungia. Alisema hadi Juni 2026, watu 27,374,283 walikuwa wamesajiliwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), wakati idadi ya laini za simu za kiganjani zilizosajiliwa ikitajwa kufikia 106,823,601.
Ndaki alisema tofauti hiyo inaashiria uwezekano wa kuwepo kwa laini zilizosajiliwa kwa kutumia vitambulisho vya watu wengine, hali inayohitaji uhakiki wa kina ili kuimarisha usalama wa mawasiliano.
Katika eneo la usimamizi wa mikopo ya miradi, kamati hiyo imeishauri serikali kupitia Wizara ya Fedha kuandaa sera na miongozo ya kudhibiti ufutwaji, usitishaji na ubadilishaji wa matumizi ya fedha za mikopo ya miradi bila kufuata taratibu zilizokubaliwa. Ndaki alisema taarifa za ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zimebaini kutokuwepo kwa sera na miongozo inayosimamia mabadiliko ya matumizi ya fedha hizo. Kamati hiyo iliishauri serikali iweke utaratibu wa kuwasilisha taarifa bungeni kuhusu mabadiliko makubwa ya matumizi ya fedha hizo na hatua zinazochukuliwa kulinda maslahi ya serikali na wananchi.

Post a Comment