DK MWINYI KUTANGAZA UTALII KOREA KUSINI
RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi anatarajiwa kuelekea nchini Korea Kusini leo kwa lengo kuu la kutangaza utalii wa visiwa na kuvutia fursa za uwekezaji katika majukwaa makubwa ya kimataifa. Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Ragey Mohamed alisema katika ziara hiyo Dk Mwinyi atatunza na kutangaza urithi wa Zanzibar wakati akitembelea Maonesho ya Dunia ya Visiwa ya Yeosu 2026 pamoja na kushiriki Jukwaa la 27 la Sera za Utalii kwa Visiwa (ITOP Forum 2026) nchini humo.
Katika maonesho hayo, Zanzibar itatumia fursa hiyo kutangaza vivutio vyake vya utalii, historia na urithi wa Kiswahili kupitia mavazi ya Kizanzibari, ngoma, muziki na vyakula vya asili ili kuvutia watalii zaidi. Maonesho hayo ya Yeosu yanayobeba kaulimbiu ya “Island, Connecting the Ocean and the Future” yatawakutanisha washiriki kutoka mataifa mbalimbali kutangaza fursa za utalii, rasilimali za bahari, utamaduni na teknolojia ya visiwa.
Akiwa nchini humo, Dk Mwinyi atashiriki majadiliano kuhusu utalii endelevu na uwekezaji akishirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii (UN Tourism). Zanzibar, ambayo ndiyo mwanachama pekee kutoka Afrika katika mtandao wa ITOP wenye wanachama 12, inajiandaa kuwa mwenyeji wa jukwaa hilo mwaka 2027 ambapo Dk Mwinyi atakabidhiwa rasmi bendera ya uenyeji huo. Pia anatarajiwa kukutana na viongozi wa kampuni za nishati, viwanda na uzalishaji wa chakula ili kuimarisha uwekezaji na uchumi wa Zanzibar.
Akiandika katika chaneli yake ya Whatsapp Leo, tarehe 25 Oktoba 2026, Rais Mwinyi alisema anaelekea nchini Korea Kusini kushiriki Jukwaa la 27 la Sera za Utalii kwa Visiwa na kutembelea Maonesho ya Dunia ya Visiwa 2026, yatakayofanyika Jijini Yeosu.
"Ushiriki wangu katika majukwaa haya ni fursa muhimu ya kuitangaza Zanzibar kimataifa, kuimarisha ushirikiano katika sekta ya utalii, kuvutia uwekezaji na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Zanzibar."
Aidha alisema;"Ninaamini kuwa ushiriki huu utafungua fursa mpya za maendeleo katika sekta ya utalii, kukuza uchumi wa Zanzibar na kuongeza fursa za ajira na ustawi wa wananchi wetu."
Post a Comment