TBS YAHADHARISHA: KUCHANGANYA POMBE NA ‘ENERGY DRINKS’ NI HATARI KUBWA KWA AFYA
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewatahadharisha wanywaji wa pombe wanaochanganya na vinywaji vya kuongeza nguvu mwilini kuwa kufanya hivyo kunahatarisha usalama wa afya zao, likisisitiza kuwa wakati bidhaa zinaweza kuwa na ubora uliothibitishwa, matumizi holela yamekuwa tishio kubwa kwa ustawi wa jamii.
Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk Ashura Katunzi, alitoa tahadhari hiyo juzi mkoani Geita wakati akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa ofisi za TBS za Kanda ya Ziwa Magharibi, ambapo alisema kuwa utafiti uliofanywa na shirika hilo ulibaini uwepo wa matumizi yasiyo sahihi ya bidhaa za pombe licha ya wazalishaji kuzingatia viwango vinavyotakiwa.
Dk Katunzi alifafanua kuwa baadhi ya watumiaji wamekuwa wakichanganya pombe na vinywaji vya kuongeza nguvu bila kung’amua kiwango halisi cha mchanganyiko huo, jambo ambalo linahatarisha mfumo wao wa fahamu na afya kwa ujumla. Akisisitiza kuhusu utaratibu sahihi wa matumizi, Mkurugenzi Mkuu huyo alisema kuwa ni vyema usinywe bila kula na kamwe usichanganye pombe na vinywaji vya kuongeza nguvu, kwani vinapoingia mwilini vinapunguza usalama wa afya.
Aliongeza kuwa wazalishaji wa pombe wanayo dhima na wajibu wa kuhakikisha wanazingatia ubora ili kufanikisha azma ya kulifikia taifa lenye vizazi vilivyo salama kuelekea Dira ya 2050, huku bidhaa yenyewe ikiendelea kuwa salama kwa matumizi yanayostahili.
Dk Katunzi alihitimisha kwa kutoa wito kwa wafanyabiashara na wananchi kuhakikisha wanafanya biashara huku wakiwalinda Watanzania, akibainisha kuwa bidhaa zinaweza kuwa na ubora lakini matumizi holela kama vile kunywa kavu na kuchanganya na energy drinks ndiyo yanayoharibu afya za wananchi, hivyo TBS itaendelea kufanya tafiti na kusimamia usalama sokoni ili kukabiliana na changamoto hiyo.
Post a Comment