AJIRA 5,000 KUPATIKANA MRADI WA TRILIONI 7.8 RUVUMA




MRADI mkubwa wa Kongani ya Viwanda unaotekelezwa na Kampuni ya Hongwang Tanzania Holdings wilayani Songea, mkoani Ruvuma, unatarajiwa kutoa zaidi ya ajira 5,000 kwa Watanzania na kuchochea kwa kasi maendeleo ya kiuchumi nchini.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Ahmed Abbas alibainisha hayo wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati, Dk Juma Homera aliyetembelea eneo la mradi huo, akieleza kuwa uwekezaji huo unaogharimu Dola za Marekani bilioni tatu, sawa na Shilingi trilioni 7.8, ni wa kimkakati na utahusisha uzalishaji wa megawati 2,000 za umeme kupitia vyanzo mbalimbali, ikiwemo makaa ya mawe, pamoja na ujenzi wa viwanda vya aluminiamu na chuma.

Mkuu huyo wa mkoa alifafanua kuwa sehemu ya umeme utakaozalishwa utatumika kuendesha viwanda vilivyopo ndani ya kongani hiyo, huku umeme utakaobaki ukiuzwa kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ili kuingizwa kwenye gridi ya taifa na kuimarisha nishati nchini. Tayari mwekezaji huyo ameanza ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha umeme huo kwenda kituo kikuu cha kupokea umeme kilichopo Songea mjini.

Akihitimisha maelezo yake, Abbas aliipongeza Serikali kwa kuweka mazingira bora yanayovutia uwekezaji wa kiwango hicho, huku akiwataka wananchi wa Ruvuma kuwa walinzi wa mradi huo na kuziomba vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kuimarisha ulinzi wa rasilimali zote zinazotumika ili mradi huo ulete tija iliyokusudiwa.

No comments