AJALI YA MOROGORO SERIKALI YAOMBA MSAADA UTAMBUZI WA MIILI




.David Mwaifuge, maarufu kama 'The Tz Tyger'alikuwamo anena


Na Mwandishi Wetu, BSKY Media

Serikali imewataka ndugu wa watu waliokuwa wakisafiri kwa basi la Kampuni ya Green Line lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Mbeya kufika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kutoa sampuli za vinasaba. 

Hatua hiyo inalenga kusaidia utambuzi wa miili 20 ya marehemu walioungua vibaya katika ajali hiyo ili iweze kukabidhiwa kwa familia husika kwa heshima na kufuata mila na taratibu zao.

Ajali hiyo ilisababisha jumla ya vifo 28 na majeruhi 30.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Queen Sendiga, alisema hayo alipowatembelea majeruhi waliokuwa wakipatiwa matibabu hospitalini hapo na kueleza kuwa moto uliotokana na ajali hiyo uliharibu miili kwa kiwango kikubwa. 

Kwa upande wake, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk Fidelice Mafumiko, alibainisha kuwa sampuli za mabaki ya miili isiyotambuliwa imepelekwa kwenye maabara jijini Dar es Salaam, huku wataalamu wawili wakibakizwa Morogoro kushirikiana na uongozi wa hospitali. 

Aliongeza kuwa sampuli kutoka kwa ndugu wa karibu kama wazazi na ndugu wa tumbo moja zitatumika kulinganisha vinasaba huku wataalamu wakifanya kazi mchana na usiku.

Kuhusu maendeleo ya majeruhi, Sendiga alieleza kuwa wengi waliopata majeraha madogo wameanza kupata nafuu na kuruhusiwa, huku serikali ikigharimia nauli zao za kurejea nyumbani, wakati majeruhi saba waliohitaji matibabu zaidi wamehamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. 



Ajali hiyo ilitokea eneo la Kikombe cha Chai, Kata ya Mkambarani Wilayani Morogoro katika Barabara ya Morogoro na Dar es Salaam, baada ya basi hilo kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa linatoka Iringa kwenda Dar es Salaam likiwa limesheheni miti ya mirunda, jambo lililosababisha basi hilo kuwaka moto. 

Kutokana na tukio hilo, Sendiga aliliagiza Jeshi la Polisi kuimarisha usimamizi wa sheria za barabarani na kuwataka TANROADS kuweka alama na vibao elekezi vinavyokosekana.

Wakizungumza kuhusu tukio hilo, baadhi ya majeruhi wamesimulia namna walivyopambana kujiokoa huku wenzao wakiteketea ndani ya basi. 

Miongoni mwa manusura hao ni msanii na mtayarishaji wa filamu, David Mwaifuge, maarufu kama 'The Tz Tyger', aliyekuwa akisafiri kwenda Mbeya kutembelea wazazi wake. 



Alieleza kuwa alikuwa amelala wakati ajali inatokea, na kwamba miti ya mirunda iliyokuwa kwenye lori ilivunja vioo na kuingia ndani ya basi kabla ya moto kuwaka. Alishuhudia wenzake wakiungua wakiwa wamenasa kwenye viti huku paa la gari likiwa limeshuka, ambapo yeye na wachache walifanikiwa kutokea dirishani lakini jirani yake aliyesafiri naye alipoteza maisha.

Manusura wengine, akiwemo Athumani Pazia aliyekuwa akielekea Uyole kwa kazi za ujenzi, pamoja na Liberata Mgulunde na Carolina Moshi, walimshukuru Mungu kwa kunusurika baada ya kufanikiwa kuvunja dirisha na kutoka kabla ya moto kusambaa. Mwaifuge alitoa wito kwa serikali na wamiliki wa vyombo vya usafiri kuimarisha usimamizi kwa madereva wa safari za usiku ili kuepuka ajali zinazotokana na uchovu na usingizi. 

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Best Magoma, alisema huduma zinaendelea kutolewa kwa majeruhi wote na aliwasihi wananchi kuendelea kuzingatia tahadhari zote za kujikinga na majanga.

No comments