Bongo Flava Honors kwenda kwa 20 percent Oktoba30
MRATIBU wa Tamasha la Bongo Flava Honors, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ amesema tamasha la Oktoba 30, litakuwa maalumu kwa ajili ya kumheshimisha msanii mkongwe Abbas Kinzasa ‘20 Percent’.
Akizungumza Dar es Salaam Sugu alisema japokuwa siku hiyo itakuwa maalumu kwa 20 Percent lakini wasanii wengine wakongwe kama Joseph Haule ‘Professor Jay’ wanatarajiwa pia kuwepo jukwaani.
“Tamasha la kufunga msimu ambalo ni maalumu kwa 20 Percent litafanyika katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki hivyo mashabiki waje kwa wingi wafurahie na wasanii wao. Lengo kuu la tamasha ni kutoa heshima na kutambua mchango mkubwa wa wasanii waliojenga tasnia ya Bongo fleva, ambapo safari hii tuzo na jukwaa kuu vinakwenda kwa mkongwe 20 Percent,” alisema. Sugu alisema 20 Percent ataimba nyimbo zake kama Tamaa Mbaya, Ya Nini Malumbano, Mama Neema, Ningekusamehe, Binti Kimanzi, Money Money, Maisha ya Bongo, Bangi Bangi na nyingine nyingi.
Alisema ngoma za msanii huyo zina ujumbe wenye mafundisho na nyingi zinaguza hisia kali iliyogusa mioyo ya mashabiki wengi. Wasanii waliotumbuiza msimu huu ni Joseph Mayanja ‘Jose Chameleone’ kutoka Uganda aliyetumbuiza na kupewa heshima yake Julai 31, mwaka huu Masaki, akiwa msanii wa kwanza wa nje ya Tanzania kupewa heshima hiyo.
Mkongwe Professor Jay alitunukiwa nishani ya heshima na kutumbuiza mwanzoni mwa msimu huu Mei Mosi, mwaka huu katika ukumbi wa 710 Kawe Garden, Dar es Salaam.

Post a Comment