MKUTANO WA 153 WA UMOJA WA MABUNGE DUNIANI IPU WAANZA ARUSHA HUKU DKT TULIA AKISISITIZA USAWA WA KIJINSI
Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani IPU, Dkt Tulia Ackson, amezitaka nchi wanachama kuhakikisha usawa wa kijinsia hauishii katika kuongeza idadi ya wanawake, bali uwape ushawishi na madaraka katika ngazi za maamuzi.
Akizungumza katika Mkutano wa 153 wa IPU Jukwaa la Wanawake katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha AICC, Dkt Tulia amesema katika kipindi chake cha uongozi IPU imefanya marekebisho ya Katiba na Kanuni zake kwa lengo la kuimarisha usawa wa kijinsia katika ngazi mbalimbali.
Amesema IPU pia imepitisha kwa mara ya kwanza Sera ya Kupinga Unyanyasaji katika Mikutano na Matukio, inayokataza aina zote za unyanyasaji, ikiwemo wa kingono, pamoja na kuweka mifumo ya kuripoti na kushughulikia vitendo hivyo.
Dkt Tulia amesisitiza kuwa wanawake wanapaswa kuwa na nafasi ya kushiriki kikamilifu katika kufanya maamuzi, akisema kuwa wanapaswa kuhakikisha kwamba usawa wa kijinsia unaenda sambamba na uwakilishi, ushiriki na fursa sawa za uongozi na kufanya maamuzi.
Aidha, amewataka washiriki wa mkutano huo kurejea katika nchi zao na kupeleka maazimio, mipango ya utekelezaji na mikakati ya usawa katika mabunge yao, huku wanaume wakishirikishwa kama wadau muhimu katika kufanikisha usawa huo.
Amesisitiza pia umuhimu wa kuwapa nafasi wanawake vijana, wanawake kutoka jamii zilizotengwa na wanawake wenye ulemavu kushiriki katika uongozi na kufanya maamuzi.
Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani IPU umeanza jijini Arusha huku ukiwakutanisha zaidi ya wajumbe elfu mbili kutoka mabunge mbalimbali duniani.
Hadi jana jioni mabunge mia moja hamsini na tatu kati ya mia moja themanini na tatu zinazounda IPU yalikuwa yamesajiliwa kushiriki mkutano huo unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha AICC, kwa siku tano.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano wa 153 wa IPU, Daniel Eliufoo alisema idadi hiyo ya mabunge yaliyothibitisha ushiriki ni kubwa na inaonesha umuhimu wa mkutano huo katika kujadili changamoto zinazoikabili dunia.
Alisema mbali na mabunge wanachama, IPU pia hushirikiana na jumuiya na vyama mbalimbali vya kibunge vya kikanda na kimataifa vinavyoshiriki kama waangalizi ikiwemo Jukwaa la Mabunge ya Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC, Bunge la Afrika, vyama vya kibunge vya nchi za Mediterranean na Jukwaa la Kibunge la Maziwa Makuu lenye makao makuu Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.
Tovuti ya IPU imeeleza katika mabunge mia moja themanini na tatu wanachama wa umoja huo asilimia ishirini na saba nukta tano ya wabunge duniani ni wanawake na asilimia kumi na tisa nukta moja ni vijana wenye umri usiozidi miaka arobaini.
Eliufoo alisema mkutano huo ni muhimu kimataifa kwa sababu unawakutanisha viongozi wa taasisi za mabunge, wakiwemo maspika, makatibu wa mabunge na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za kimataifa kujadili masuala mbalimbali na changamoto za kimataifa.
Alisema mkutano wa 153 wa IPU una kaulimbiu inayolenga kuimarisha utawala bora na kushirikisha jamii kupitia imani na ujumuishi, huku masuala ya wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na makundi mengine yakipewa nafasi katika mjadala utakaohusisha matumizi ya teknolojia, hususani akili bandia, mabadiliko ya tabianchi, agenda za vijana na masuala ya jinsia.
Alisema mkutano huo utaiweka Tanzania katika ramani ya kimataifa na kuongeza nafasi ya Tanzania kujitangaza kidiplomasia, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni kupitia ujio wa zaidi ya wajumbe elfu mbili watakaohitaji huduma mbalimbali zikiwemo malazi, chakula, usafiri na kutembelea maeneo ya utalii nchini na Kituo Cha Urithi wa Utamaduni jijini Arusha.
Katika mkutano huo tarehe tisa Oktoba, mwaka huu unatarajiwa kumchagua Rais wa thelathini na mbili wa IPU kuchukua nafasi ya Rais wa sasa Dk Tulia Ackson ambaye alichaguliwa katika Mkutano wa 147 wa IPU uliofanyika Luanda nchini Angola mwaka 2023.
Mtaalamu wa masuala ya diplomasia katika Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dk Salim Ahmed Salim CFR, Godwin Amani alisema diplomasia ya mikutano ni eneo muhimu ambalo nchi inaweza kulitumia kuimarisha uhusiano na mataifa mengine, kutengeneza marafiki wapya na kupenyeza ajenda zake.
Kwa upande wake, mtaalamu wa masuala ya uchumi katika Chuo Kikuu cha Dodoma UDOM, Dk Paul Loisulie alisema mkutano huo unaweza kuiletea Tanzania faida ikiwemo ya kuimarisha biashara, uwekezaji, utalii na ushirikiano wa kiuchumi kupitia mikataba baina ya nchi na kujenga imani kwa wageni na washiriki.



Post a Comment