Ndejembi: Teknolojia ni Nguzo Muhimu kuleta Ufanisi Kodi za Ndani




Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema kuwa matumizi ya teknolojia ni nyenzo muhimu ya kusaidia katika kukusanya mapato ya ndani kwa ufanisi na haki, jambo litakalowezesha nchi kufadhili shughuli zao na vipaumbele vya maendeleo kupitia rasilimali za ndani.

Mhe. Ndejembi ametoa wito huo leo, Oktoba 6, 2026, jijini Arusha, wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika ufunguzi wa Mkutano wa 46 wa Chama cha Wasimamizi wa Kodi wa Jumuiya ya Madola (CATA) unaofanyika katika Ukumbi wa Gran Melia.

Amesema kuwa mfumo mzuri wa kodi unapaswa kuwa wa uhakika, kuwezesha biashara halali, kuhimiza uwekezaji na urasimishaji, na kuiwezesha sekta binafsi kutumia nafasi yake ya kuchagiza mabadiliko ya kiuchumi kama ilivyokusudiwa chini ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Tanzania 2050, huku akisisitiza kuwa ukusanyaji wa kodi haupaswi kuzuia shughuli za kiuchumi zenye tija bali unapaswa kuziuunga mkono.

Akizungumzia kuhusu ujenzi wa uchumi endelevu, Makamu wa Rais alibainisha kuwa ukuaji wa mapato lazima utokane na upanuzi wa wigo wa kodi, ulipaji kodi kwa hiari, matumizi bora ya data na teknolojia, pamoja na mfumo wa kodi unaokua sambamba na uchumi. Aliongeza kuwa kupitia bajeti ya mwaka 2026/27, Tanzania inatarajia kukusanya mapato ya kodi ya Shilingi trilioni 36.99, huku mapato ya ndani yakitarajiwa kufadhili takriban asilimia 74.2 ya bajeti ya Taifa, hali inayoashiria hatua kubwa kuelekea kujitegemea kiuchumi.

Katika hatua nyingine, Mhe. Ndejembi alieleza kuwa Tanzania inatambua umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya kodi, akitolea mfano wa Julai 2026 ambapo nchi ilitajwa kimataifa kuwa inafuata vigezo vya uwazi na kubadilishana taarifa zinapohitajika. Alisisitiza kuwa ushirikiano huo unasaidia kulinda mapato na kupunguza hatari ya utozaji kodi mara mbili kwa wawekezaji halali.

Kwa upande wake, Rais wa CATA, Dkt. Abu Tariq Jamaluddin, aliisifu jumuiya hiyo kwa kuendelea kuimarisha programu za uongozi, teknolojia, na kubadilishana uzoefu ili kufikia utawala bora wa kodi, kauli iliyoungwa mkono na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), CPA Yusuph Mwenda, aliyemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake thabiti katika mabadiliko ya kidijitali, yakiwemo mafanikio ya Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Mapato ya Ndani (IDRAS) na utoaji wa ankara za kielektroniki.

Mkutano huo wa siku tano unawakutanisha wataalamu na viongozi zaidi ya 400 kutoka nchi 48 za Jumuiya ya Madola chini ya kauli mbiu isemayo "Kutumia Teknolojia kwa Ukusanyaji Bora wa Mapato", ukilenga kubadilisha maarifa na uzoefu katika kuongeza ufanisi kupitia mifumo ya kisasa ya kidijitali.

No comments