SPIKA ZUNGU ATOA WITO KWA MABUNGE DUNIANI KUTEKELEZA MAAZIMIO YA IPU KWA VITENDO


Na Ripota wa TBN


Tanzania imetoa wito kwa mabunge duniani kuhakikisha maazimio yanayopitishwa na Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) yanatekelezwa kwa vitendo kupitia sheria, sera na hatua madhubuti zinazoboresha maisha ya wananchi. 

Wito huo ulitolewa na Spika wa Bunge, Mussa Zungu wakati wa kufunga mkutano huo uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), ambapo alisisitiza kuwa mafanikio ya maazimio hayo yanapaswa kupimwa kwa mabadiliko yanayoonekana katika maisha ya watu badala ya kuishia kwenye maandishi tu.

Spika Zungu alieleza kuwa licha ya tofauti za kisiasa na kitamaduni zilizopo miongoni mwa nchi wanachama, mabunge yanapaswa kuendeleza umoja, mazungumzo na ushirikiano badala ya kutelekea kwenye migawanyiko na migogoro. 

Alisisitiza umuhimu wa ujumuishi ili maamuzi ya IPU yawe na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi. 

Katika hatua nyingine, alimpongeza Spika wa Bunge la Wawakilishi la Australia, Milton Dick, aliyechaguliwa kuwa Rais mpya wa IPU akimrithi Dk. Tulia Ackson, huku akiwashukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Watanzania na wakazi wa Arusha kwa ukarimu wao kwa wajumbe.

Kwa upande wake, Rais aliyemaliza muda wake wa miaka mitatu, Dk. Tulia Ackson, alisema ameridhishwa na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chake cha uongozi ambapo alifanya maboresho kadhaa ya kuimarisha utendaji na ushiriki wa makundi mbalimbali katika demokrasia. 

Maboresho hayo yalijumuisha kuipa nafasi ya Makamu wa Rais majukumu rasmi ya Naibu Rais, kupunguza umri wa kundi la wabunge vijana hadi chini ya miaka 40, na kubadilisha kanuni ili kuongeza uwakilishi wa wanawake uliofikia takribani asilimia 39, pamoja na kupitisha sera ya kupambana na unyanyasaji wakati wa mikutano.

Dk. Tulia alihitimisha kwa kueleza kuwa ujenzi wa demokrasia ni mchakato endelevu na hakuna uongozi unaoweza kukamilisha kila jambo kwa wakati mmoja. 

Alibainisha kuwa huo ulikuwa mkutano wake wa mwisho kuhutubia wajumbe akiwa Rais wa chombo hicho, na aliahidi kuendelea kuwa balozi wa IPU na kuwa tayari kumshauri pamoja na kumsaidia mrithi wake, Milton Dick, katika majukumu yake mapya.

No comments