DC MPOGOLO ATAKA KASI MIRADI YA MIUNDOMBINU KABLA YA VULI




Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya miundombinu katika Wilaya ya Ilala kuongeza kasi ya kazi bila kuathiri ubora, ili miradi ikamilike kwa wakati na kuwahi msimu wa mvua.

Mpogolo ameyasema hayo leo wakati akikagua miradi mbalimbali ya barabara na madaraja inayoendelea katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, ikiwemo ujenzi wa Daraja la Majumba Sita pamoja na barabara yenye urefu wa kilomita tatu, inayounganisha Kata ya Kipawa na Segerea. Mradi huo unatekelezwa na Jiangxi Geo Engineering Corporation, chini ya usimamizi wa Mhandisi Mshauri M/s Mhandisi Consultancy.

“Tunataka miradi ikamilike haraka, lakini hatutaki kasi ije kwa gharama ya ubora. Wakandarasi waongeze kasi na ikiwezekana wafanye kazi usiku na mchana ili kuwahi msimu wa mvua na wananchi waanze kunufaika na miundombinu hii,” amesema Mpogolo.

Katika ziara hiyo, Mpogolo pia amekagua Barabara ya Banana–Kitunda–Kivule hadi Msongola, ambapo tayari kazi ya uwekaji wa lami imeanza, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuboresha mtandao wa barabara na kurahisisha usafiri kwa wananchi.

Ameipongeza TARURA, wakandarasi na wahandisi kwa kazi inayoendelea, huku akisisitiza kuwa changamoto zinazoweza kuchelewesha utekelezaji, ikiwemo masuala ya fidia, zinapaswa kushughulikiwa kwa haraka.


No comments