SAMIA KUFUNGUA RASMI BWAWA LA JULIUS NYERERE

 



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP), chenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115, Agosti 22, 2026, katika eneo la mradi Rufiji, Mkoa wa Pwani.

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema hayo  Agosti 15, 2026 jijini Dar es Salaam.

Amesema JNHPP ni mradi mkubwa zaidi wa kuzalisha umeme nchini uliotekelezwa kwa fedha za ndani, ukiwa na uwekezaji wa takribani shilingi trilioni 7.452, sawa na Dola za Marekani bilioni 3.35. Mradi huo ulianza kujengwa Juni 2019 na kukamilika Machi 2025.

Kwa mujibu wa Ndejembi, hadi Mei 31, 2026, JNHPP ilikuwa imezalisha takribani asilimia 44.9 ya umeme wote uliozalishwa na kuingizwa katika Gridi ya Taifa kwa kipindi cha mwaka mmoja, hivyo kuchangia karibu nusu ya umeme unaotumika nchini na kusaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa umeme.

Ameongeza kuwa mbali na uzalishaji wa umeme, mradi huo wenye bwawa lenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo bilioni 33 za maji, unatarajiwa kusaidia kudhibiti mafuriko katika Mto Rufiji, kilimo cha umwagiliaji, utalii na matumizi ya binadamu.

Ndejembi amesema mradi wa JNHPP pia unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na amewaalika Watanzania kufuatilia na kushiriki katika uzinduzi huo, akieleza kuwa ni tukio la kihistoria katika maendeleo ya sekta ya nishati nchini.

No comments