DC MPOGOLO ATOA SIKU 14 MKANDARASI KUKAMILISHA BARABARA YA MUHIMBILI
Mkuu wa Wilaya ya Ilala,
Edward Mpogolo, amempa mkandarasi China Wu Yi Construction siku 14 kuhakikisha
uwekaji wa lami umeanza katika barabara inayopita eneo la Hospitali ya Taifa
Muhimbili, huku akiagiza TARURA na TAKUKURU kufuatilia kwa karibu utekelezaji
wa mradi huo wa DMDP II Package IV wenye thamani ya Shilingi bilioni 26.06.
Akizungumza wakati wa ziara
ya kukagua mradi huo wenye urefu wa kilomita 7.38 unaohusisha barabara 16,
Mpogolo amesema kuwa barabara ya Muhimbili ni muhimu sana kwa wagonjwa na
wananchi, hivyo haiwezi kuendelea kucheleweshwa wakati Serikali imekwisha kutoa
zaidi ya Shilingi bilioni 5.
“Nataka ndani ya siku 14
barabara hii iwe imeanza kumwagwa lami. Meneja wa TARURA Wilaya ya Ilala
simamia hili. Pia nataka TAKUKURU Wilaya ya Ilala ifuatilie commitment hii na
kuhakikisha kila mmoja anawajibika kwa nafasi yake. Baada ya siku 14 tutarudi
hapa kuona kazi iliyofanyika,” amesema Mhe. Mpogolo
Amesema kuwa pamoja na muda
wa mradi kuongezwa kutoka Agosti 14 hadi Desemba 16, 2026, hilo halimpi
mkandarasi sababu ya kufanya kazi kwa kusuasua, na kumtaka kuongeza mitambo,
vifaa, wataalamu, pamoja na kufanya kazi mchana na usiku.
“Serikali imelipa fedha.
Tunachotaka sasa si maelezo, tunataka matokeo. Ongezeni vifaa, ongezeni watu,
ongezeni zamu na mfanye kazi usiku na mchana. Mradi huu ni wa wananchi na
lazima tuone thamani ya fedha zao,” amesema.
Hadi sasa, mradi umefikia
takribani asilimia 55 ya utekelezaji, huku Serikali ikiwa tayari imelipa zaidi
ya Shilingi bilioni 5.
Aidha, amemtaka Mhandisi
Mshauri, M/s Mhandisi Consultancy, kuwasilisha vielelezo vyote vya maandishi
alivyomwandikia mkandarasi kutokana na kuchelewa kwa kazi hiyo, akisisitiza kuwa
wasimamizi hao wanalipwa kupitia fedha za mradi na wanapaswa kuwajibika
kikamilifu ili kuhakikisha wananchi wanapata thamani halisi ya fedha za umma.
“Tusilaumu Mkandarasi peke
yake. Mhandisi Mshauri naye ana wajibu wake. Serikali inamlipa kupitia fedha za
mradi ili asimamie kazi na kuhakikisha Mkandarasi anafanya kazi kwa mujibu wa
mkataba. Nataka kuona barua na maelekezo yote uliyompa Mkandarasi, hatua ulizochukua
na commitment yako ya kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati. Kila mmoja
atawajibika kwa nafasi yake,” amesisitiza Mhe. Mpogolo.»
Ameongeza kuwa usimamizi wa
mradi haupaswi kuishia kwenye nyaraka pekee, bali unapaswa kuonekana kupitia
kasi ya kazi, ubora wa utekelezaji na matokeo yanayopatikana eneo la mradi.
“Unalipwa kwa ajili ya
kusimamia. Tunataka usimamizi unaoonekana kwenye matokeo, si kwenye karatasi
pekee. Commitment yako lazima ionekane kwenye kasi ya kazi ya Mkandarasi,”
amesema.
Mhe. Mpogolo amesisitiza
kuwa Meneja wa TARURA Wilaya ya Ilala pamoja na Mhandisi Mshauri wanapaswa
kuongeza ufuatiliaji wa utekelezaji wa mradi na kuhakikisha maagizo
yanayotolewa kwa Mkandarasi yanatekelezwa kwa wakati.
Mhe. Mpogolo ameeleza kuwa
Wilaya ya Ilala itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa Mradi wa DMDP
II Package IV ili kuhakikisha fedha za Serikali zinakwenda sambamba na thamani
ya kazi inayofanyika na wananchi wanapata barabara bora kwa wakati.
Mradi wa DMDP II Package IV
unahusisha ujenzi wa barabara 16 zenye urefu wa jumla ya kilomita 7.38, kwa
gharama ya Shilingi bilioni 26.06, ukiwa unatekelezwa na China Wu Yi
Construction.

Post a Comment