TANZANIA NA DRC ZAKUBALIANA KUONGEZA KASI YA MIRADI YA UCHUKUZI NA BIASHARA





Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimefikia makubaliano rasmi ya kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya uchukuzi inayounganisha nchi hizo mbili kwa lengo la kupunguza muda na gharama za usafirishaji wa mizigo sambamba na kupanua wigo wa biashara na uwekezaji kwa manufaa ya pande zote mbili. 

Makubaliano hayo yamefikiwa leo katika Ikulu Ndogo iliyopo Zanzibar wakati wa mazungumzo rasmi kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mheshimiwa Félix Tshisekedi, ambaye yuko nchini kwa mwaliko maalum wa Rais Dkt. Samia.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Samia amesisitiza umuhimu mkubwa wa kuimarisha mtandao wa reli, barabara, huduma za bandari, na usafiri wa majini unaounganisha Bandari ya Dar es Salaam na maeneo ya uzalishaji nchini DRC kupitia Ziwa Tanganyika, akibainisha kuwa lengo kuu ni kurahisisha usafirishaji wa mizigo na kuchochea ukuaji wa kiuchumi. 

Alieleza kuwa DRC ni miongoni mwa watumiaji wakubwa wa bandari za Tanzania, ikiwa imepitisha takribani tani milioni 7.2 za mizigo mwaka 2023, na kuongeza kuwa Tanzania inaendelea kuboresha miundombinu yake ya bandari katika Ziwa Tanganyika, kuongeza idadi ya meli, na kuendeleza mtandao wa reli kuelekea Magharibi. Vilevile, alipongeza ujenzi wa barabara ya kilomita 450 inayofanywa na DRC kutoka Manono hadi Bandari ya Kalemie sambamba na uboreshaji wa bandari hiyo kupitia Ushoroba wa Kati.






Viongozi hao pia wamejadili fursa za kupanua ushirikiano katika sekta za mawasiliano, nishati, na madini, ambapo Rais Dkt. Samia ametoa wito wa kushirikiana katika uchimbaji, uongezaji thamani, utafiti, na masoko ya madini, huku akitoa mwaliko kwa DRC kujiunga na Kituo cha Madini na Jiosayansi cha Afrika kilichopo Tanzania. 

Aidha, Tanzania imeeleza utayari wake wa kupanua wigo wa biashara ya mazao ya kilimo, mifugo, na uvuvi na DRC, pamoja na kutoa huduma za kibingwa na kuendesha kambi za matibabu nchini humo, huku akisisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuunga mkono juhudi za DRC za kurejesha amani na utulivu Mashariki mwa nchi hiyo.

Kwa upande wake, Rais Tshisekedi ametangaza kuwa DRC imeanza maandalizi rasmi ya kujenga bandari kavu jijini Dar es Salaam itakayotoa huduma za forodha, usimamizi wa mizigo ya baharini, uthibitishaji wa madini, na udhibiti wa ubora wa bidhaa ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo ya nchi hiyo. 

Vilevile, amesema serikali yake inatathmini uwezekano wa kupanua safari za Shirika la Ndege Tanzania nchini DRC ili kuimarisha usafiri, utalii, na mwingiliano wa wananchi, huku akisisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuchakata na kuongeza thamani ya rasilimali zao ndani ya bara ili kujenga minyororo ya uzalishaji na kutengeneza ajira zaidi kwa vijana. 

Ziara hiyo imeweka msukumo mpya wa kiuchumi kwa nchi zote mbili ambazo ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC, zikiwa na uhusiano wa kihistoria unaounganisha bandari za Tanzania na soko lenye zaidi ya watu milioni 100 nchini DRC.


No comments