Watanzania wahimizwa kuchangamkia zabuni Afcon 2027




WATANZANIA wenye uwezo na sifa stahiki wamehimizwa kuchangamkia fursa mbalimbali za zabuni zilizotangazwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuelekea maandalizi na uendeshaji wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027). 

Akitoa taarifa hiyo Dar es Salaam juzi, Katibu wa Kamati ya Ndani, Neema Msitha alisema CAF imetangaza fursa mbalimbali za zabuni zinazohusiana na maandalizi na uendeshaji wa mashindano yake. 

Zabuni hiyo pia inahusisha maandalizi na uendeshaji wa michuano ya Afcon 2027 ambayo Tanzania itaandaa kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.

 “Kamati inawahimiza Watanzania wenye uwezo, sifa na nia ya kushiriki fursa hizi kufuatilia matangazo rasmi ya zabuni hizo kupitia tovuti ya CAF ambayo ni https://www.cafonline.com/inside-caf/ about-us/tenders/tenders-tab/ ili kusoma masharti ya kila zabuni na kuwasilisha maombi yao kufuatana na taratibu na muda uliowekwa na shirikisho hilo,” alisema Msitha.

Alieleza fursa hizo zinahusisha michezo, biashara, huduma za kitaalamu, teknolojia, masoko, usafirishaji na malazi pamoja na huduma nyingine zitakazohitajika kulingana na matakwa ya kila zabuni.

 “Tunawajulisha Watanzania, taasisi, kampuni na wadau wenye uwezo na sifa stahiki kuwa CAF imetangaza fursa mbalimbali za zabuni zinazohusiana na maandalizi na uendeshaji wa mashindano yake, ikiwamo Afcon 2027,” alieleza. 

Akihitimisha taarifa hiyo, Msitha alisema Tanzania iko tayari kwa ajili ya mashindano hayo na kuwataka Watanzania kuchangamkia fursa zinazojitokeza.

No comments