Adhabu Kali Zatolewa kwa Argentina na Hispania Vurugu Fainali ya Kombe la Dunia




Shirika la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) limetoa adhabu kali kwa wachezaji watatu wa Argentina na mmoja wa Hispania kutokana na kuhusika kwao katika vurugu zilizotokea mara baada ya kumalizika kwa fainali ya Kombe la Dunia kati ya nchi hizo mbili iliyochezwa kwenye Uwanja wa MetLife mjini New Jersey, Marekani. 

Kamati ya Nidhamu ya FIFA imemfungia mchezaji Leandro Paredes wa Argentina mechi 10 na beki Nahuel Molina mechi saba, huku wachezaji wote wawili wakitozwa faini nzito pamoja na wenzao Thiago Almada wa Argentina na Pablo Gavira ‘Gavi’ wa Hispania waliofungiwa mechi moja kila mmoja kutokana na makosa hayo ya kinidhamu uwanjani. 

Vurugu hizo zilizuka mara baada ya kipenga cha mwisho, ambapo Paredes alihusika moja kwa moja kwa kumshika shingoni na kumwangusha mchezaji Eric Garcia wa Hispania, tukio ambalo limechangia adhabu yake kuwa kubwa zaidi miongoni mwa wote waliohusika katika sakata hilo. 

Mbali na wachezaji, adhabu hiyo pia imemkuta Kocha Msaidizi wa Argentina, Roberto Ayala, ambaye amefungiwa mechi tatu kwa kukiuka kanuni za nidhamu, huku Shirikisho la Mpira wa Miguu la Argentina (AFA) likitozwa faini kubwa na kuwekewa masharti ya kucheza mechi mbili zijazo za nyumbani huku mashabiki wakiingia kwa nusu ya uwezo wa uwanja huo. 

Kufuatia maamuzi hayo, uongozi wa AFA umesema kuwa utakata rufaa dhidi ya adhabu hizo zote kwa lengo la kupunguza vifungo vya wachezaji wao Paredes na Molina, na endapo rufaa hiyo itashindikana, shirikisho hilo lipo tayari kupeleka suala hilo kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) ili kupata haki.

No comments