Yatosha! Takwimu Zaweka Wazi Ukweli Kuhusu Bandari ya Dar es Salaam




Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amewatoa hofu Watanzania na kuondoa wasiwasi dhidi ya kauli za baadhi ya wanasiasa na mitandaoni zinazodai kuwa Bandari ya Dar es Salaam inakufa, huku akisisitiza kuwa takwimu za kisayansi zinaonyesha ongezeko kubwa la mizigo na ufanisi mkubwa wa upakuaji.

Akizungumza mwishoni mwa wiki na wananchi wa Jimbo la Ubungo wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu yake ya miezi nane tangu Novemba 2025 hadi Julai 2026, Profesa Kitila alieleza kuwa uwezo wa kuhudumia mizigo nchini umeongezeka kutoka tani milioni 20.78 mwaka 2021/2022 hadi kufikia tani milioni 39.90 mwezi Machi, huku mizigo ya transit kwenda nchi jirani za DRC, Zambia, Malawi, Rwanda na Uganda ikipanda kutoka tani milioni 7.4 hadi tani milioni 15.5.

Aliongeza kuwa ujio wa mwekezaji mwaka 2023/24 haukuwa wa kuuza bandari bali ulikuwa ni kuboresha uendeshaji, jambo ambalo limesaidia kupunguza muda wa kushusha mizigo kutoka saa 300 zilizokuwa sawa na zaidi ya siku kumi hadi kufikia saa 28 pekee, na kuifanya bandari hiyo kuingia kwenye orodha ya bandari kumi bora barani Afrika.

Pamoja na hayo, mbunge huyo alieleza mafanikio katika sekta ya miundombinu jimboni humo ikiwemo kukamilika kwa ujenzi wa barabara za Kimara-Korogwe hadi Mbezi Mfereji zenye urefu wa kilometa 9.2, Kifuru kilometa 1.4, Ubungo External hadi Kigogo kilometa 7.4, na Kinyerezi hadi Bonyokwa, wakati ujenzi wa barabara ya Kimara-Mafurusa-Bonyokwa hadi Kinyerezi yenye urefu wa kilometa nane ukiendelea.

No comments