VIJANA WAAMBIWA NI WAKATI KUBADILISHA UBUNIFU KUWA UTAJIRI



Maonyesho ya Mashariki Creative Economy Expo 2026 yaliyohitimishwa hivi karibuni katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam yalikuwa zaidi ya jukwaa la burudani na badala yake yaligeuka kuwa chuo kikuu cha wazi cha uchumi wa ubunifu, ambapo viongozi, wataalamu na nguli wa tasnia hiyo walijadiliana kwa kina jinsi ya kuwafanya vijana wanaoahangaika mitaani kutafuta ajira kujikita kwenye sanaa na ubunifu kama njia thabiti ya kujiletea maendeleo na kuliingizia taifa tija. 

Katika maonyesho hayo yaliyoratibiwa na Culture and Development East Africa, watoa mada na viongozi walisisitiza kwa dhati kuwa imefika wakati wa kubadilisha dhana potofu na kuona ubunifu sio tu kama kipaji cha kupitisha wakati, bali ni mali yenye thamani halisi inayoweza kuuzwa na kuingiza mapato makubwa kwenye soko la ndani na kimataifa.

Wito mkubwa unatolewa kwa vijana wengi wanaoendelea kuhangaika wakitafuta ajira rasmi kugeukia fursa za kipekee zinazopatikana kupitia mifumo iliyowekwa na serikali na taasisi zake, badala ya kukaa na kusubiri. 

Sheria na mifumo ya nchi imetoa fursa nzuri ikiwemo mikopo ya asilimia kumi inayotolewa kupitia halmashauri kwa ajili ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, pamoja na mifuko maalumu ya uendelezaji utamaduni na sanaa ambayo mara nyingi haitumiki ipasavyo na walengwa. 

Vijana wanapaswa kuacha kulalamika na badala yake kuunda vikundi rasmi, kusajili kazi zao na kuomba mikopo hiyo ili kujipatia mitaji ya kuanzisha miradi ya ubunifu kama vile studio za kisasa, vikundi vya filamu, ushonaji wa ubunifu, na usambazaji wa kazi za sanaa kidijitali.

Katika mijadala iliyofanyika wakati wa tamasha hilo, viongozi kama Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Kiswahili la Taifa, Profesa Martin Mhando, na Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Sanaa la Taifa, Profesa Saudin Mwakaje, walisisitiza kuwa thamani ya mbunifu haipaswi kubaki kwenye karatasi bali inapaswa kunaswa sokoni kupitia mifumo madhubuti ya kisheria na kibiashara. 

Profesa Mwakaje alionya wazi kuwa sera bora za uchumi wa ubunifu sharti zimsaidie msanii kulinda kazi zake dhidi ya wizi na matumizi yasiyo halali huku akijenga mnyororo rasmi wa uchumi. Sambamba na hilo, mwanamuziki nguli wa kimataifa kutoka Afrika Kusini, Yvonne Chaka Chaka, aliyewasili kwenye maonyesho hayo, aliwahimiza vijana kujikita katika elimu, nidhamu, na kurasimisha shughuli zao ili waweze kushirikiana na wasanii wakubwa kimataifa na kufungua milango mipya ya masoko ya kikanda.

Hali kadhalika, viongozi wengine akiwemo Mwenyekiti wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Mona Mwakalinga, na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania, Bi. Naomi Mungure, walisisitiza kuwa biashara ya haki miliki ndiyo uti wa mgongo wa mafanikio ya msanii yeyote duniani. Kupitia ushirikiano wa karibu na taasisi hizi, vijana wanafundishwa namna ya kulinda kazi zao, kuvutia uwekezaji mkubwa, na kutumia lugha ya Kiswahili na utamaduni wetu kama bidhaa za thamani kubwa ya kibiashara. 

Ni dhahiri kuwa mafanikio ya Maonyesho ya Mashariki Creative Economy Expo 2026 yanatoa changamoto kwa vijana wetu kubadilisha mtazamo, kuchangamkia mikopo ya halmashauri na mifuko ya utamaduni, na kuanza safari ya kujiletea tija ya kiuchumi kupitia vipaji vyao mikononi mwao.

No comments