TFF YAMFUNGIA MMILIKI WA AZAM FC




KAMATI ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemfungia mmiliki wa Azam FC, Jamal Bakhresa kutojihusisha na mpira kwa kipindi cha mwaka mmoja. 

Taarifa ya TFF iliyotolewa jana imeeleza hatua hiyo ni baada ya kutiwa hatiani kwa utovu wa nidhamu ambapo Bakhresa mbele ya TFF alikiri kutenda makosa na kuahidi kutorudia. 

Taarifa hiyo ilieleza kamati ilimtia hatiani kwa kuzingatia Ibara ya 11(f) ya Kanuni za Nidhamu za TFF, Toleo la 2021.

TFF imesema Bakhresa alitenda makosa kabla na baada ya mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, kati ya Simba dhidi ya Azam uliopigwa Zanzibar. Taarifa iliyotolewa na TFF ilisema: “Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemfungia Kiongozi wa Azam FC, Jamal Bakhresa kujishughulisha na mpira wa miguu kwa kipindi cha mwaka mmoja.” 

Iliongeza: “Bakhresa ametiwa hatiani kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu alivyofanya kabla na baada ya mechi ya Fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB iliyochezwa kisiwani Pemba.” 

Mlalamikiwa alikiri kufanya makosa mbele ya kamati hiyo iliyoongozwa na Wakili Alex Mushumbusi kwa malalamiko yote mawili yaliyowasilishwa dhidi yake. 


No comments