WAZEE DAR WAONYA VIJANA KUJIHUSISHA NA MAANDAMANO
Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam wametoa wito kwa vijana kutoshiriki maandamano yanayopangwa kufanyika Julai 7, 2026, wakisisitiza kuwa Tanzania imeendelea kudumisha amani kwa muda mrefu na kwamba changamoto za kisiasa zinapaswa kutatuliwa kwa njia zilizopo ikiwemo za kisheria na kupitia uchaguzi mkuu.Akizungumza na wanahabari Ijumaa Julai 3, 2026, Rehema Nyadundo amesema hakuna sababu ya vijana kushawishiwa kushiriki maandamano wakati nchi ina amani na utulivu, akibainisha kuwa endapo wananchi hawaridhishwi na uongozi uliopo wanapaswa kusubiri uchaguzi mkuu badala ya kuingia mitaani.
Ameongeza kuwa Serikali inapaswa kuchukua hatua dhidi ya watakaovunja sheria, huku akiwataka wazazi kuwajibika na kuwalea watoto wao katika maadili mema ili kuepusha kushiriki katika maandamano yasiyo halali.
Kwa upande wake, Mzee Benjamin Ndauka amewataka vijana kulinda amani ya nchi na kutoingia kwenye vurugu, akisema maendeleo yanayoonekana nchini yanapaswa kuwa msingi wa kuendelea kudumisha utulivu na mshikamano wa kitaifa.
Amesema wanaohamasisha maandamano wanapaswa kuangalia hali halisi ya maendeleo nchini, akieleza kuwa huduma kama hospitali, masoko, shule na barabara zinaonyesha hatua zilizopigwa chini ya uongozi wa sasa.
Naye Mzee Juma Mikoba amesema baadhi ya watu wanaiga mwenendo wa mataifa ya Ulaya kwa kuhamasisha maandamano, jambo ambalo halipaswi kupewa nafasi nchini, akisisitiza kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa za maendeleo hivyo hakuna sababu ya kuhatarisha amani iliyopo.

Post a Comment