Uchumi wa buluu: Fursa mpya kwa vijana kupitia uhifadhi wa mazingira
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, amewahimiza wananchi na hasa vijana kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazotokana na uhifadhi wa mazingira ili kujipatia kipato na kukuza maendeleo.
Dkt. Muyungi ametoa wito huo Julai 15, 2026, alipofanya ziara ya kikazi katika Kituo cha Kuendeleza Ukuzaji Viumbe Maji cha Ruhila kilichopo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, ambapo amejionea namna mradi huo unavyochagiza sekta ya uchumi wa buluu kupitia ufugaji wa samaki.
Amesema hifadhi endelevu ya mazingira imegeuka kuwa fursa muhimu, akibainisha kuwa teknolojia ya kugeuza taka kuwa chakula cha samaki ni njia madhubuti ya kusafisha mazingira huku ikitengeneza kipato kwa vijana watakaojikita katika usimamizi wa taka hizo.
Dkt. Muyungi ameongeza kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inatekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo nguzo yake ya tatu inajikita katika hifadhi ya mazingira, hatua inayolenga kuhakikisha Sera ya Uchumi wa Buluu inatekelezwa kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Ruhila, Bw. Lucka Mgwena, amesema kituo hicho kinachosimamiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kinaendelea kuibua teknolojia rafiki za uzalishaji ambazo zinaunga mkono juhudi za Serikali katika kukuza uchumi.
Bw. Mgwena amebainisha kuwa kupitia mradi huo, wafugaji wanawezeshwa kupata vifaranga bora vya samaki na teknolojia ya kuzalisha vyakula kwa kutumia taka oza kutoka kwenye mabaki ya vyakula, jambo linalosaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuongeza tija katika sekta ya uvuvi kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.



Post a Comment