BEI YA MAFUTA KUSHUKA TARATIBU


Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waagizaji Mafuta Tanzania (TAOMAC), Raphael Mgaya, amesema bei za mafuta ghafi katika soko la dunia zinaendelea kushuka taratibu, lakini mabadiliko hayo hayawezi kuonekana mara moja katika soko la ndani kutokana na mfumo wa uagizaji unaotumika nchini.


Mgaya amesema mafuta huagizwa takribani miezi miwili kabla ya kuingia sokoni, jambo linalosababisha bei za ndani kuendelea kuakisi gharama za ununuzi wa awali hata pale bei za kimataifa zinapobadilika.

Ameeleza kuwa wananchi wengi wamekuwa wakitarajia kushuka kwa haraka kwa bei za mafuta nchini mara tu baada ya kupungua kwa mivutano ya kisiasa katika maeneo yanayoathiri soko la dunia, ikiwemo Mashariki ya Kati.

Hata hivyo, amesema matarajio hayo hayazingatii muda wa mzunguko wa biashara ya mafuta.

Mgaya amefafanua kuwa hata wakati mvutano kati ya mataifa kama Marekani, Israel na Iran ulipoanza mwishoni mwa Februari, athari zake hazikuonekana mara moja nchini.

Badala yake, mabadiliko ya bei yaliibuka baadae, kuanzia Aprili na kuendelea Mei, kutokana na mafuta yaliyokuwa tayari yameagizwa kabla ya mabadiliko ya bei za dunia.

No comments