WAZIRI MKUU AONYA VIJANA DHIDI YA VURUGU
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amesema kuna watu wanaolipwa fedha kutoka nje ya nchi kwa lengo la kuwachochea vijana wa Tanzania kufanya vurugu na kushiriki katika vitendo vinavyohatarisha usalama wa nchi, akisisitiza kuwa Serikali haitavumilia matendo yanayohatarisha maisha ya wananchi.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo Julai 1, 2026 kwenye Viwanja vya Sokoine, Mugumu, wilayani Serengeti mkoani Mara, Waziri Mkuu amesema watu hao hujinufaisha kifedha huku wakiwatumia vijana kutekeleza vitendo vya vurugu.
Ameongeza kuwa vyombo vya dola tayari vimewakamata baadhi ya watuhumiwa ambao, kwa mujibu wa maelezo yake, walikiri kulipwa kati ya shilingi milioni tatu na tano kwa mwezi ili kuwahamasisha vijana kushiriki katika vitendo hivyo.
Dk Mwigulu pia amedai kuwa mmoja wa watuhumiwa kutoka mikoa ya kusini alikuwa akitengeneza vilipuzi vya asili kwa malipo, huku akiahidiwa fedha zaidi endapo angefanikiwa kuwashawishi vijana kushiriki katika vurugu.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu amewataka vijana kutokubali kutumiwa na watu wanaowashawishi kushiriki katika vitendo vya uhalifu kwa manufaa ya wengine, akisisitiza kuwa kila mmoja ana wajibu wa kulinda amani na usalama wa taifa.

Post a Comment