VYOMBO VYA HABARI VYA MTANDAONI KINARA UWASILISHAJI KAZI SAMIA KALAMU 2026 AWARDS

 



 

Hadi kufikia Jumatatu, tarehe 15 Juni 2026, jumla ya kazi za kushindanishwa 624 zimekwishawasilishwa kutoka sehemu mbalimbali nchini kupitia mfumo wa kidijitali wa samiaawards.tz kwa ajili ya kuwania Tuzo za Uandishi wa Habari na Makala za Maendeleo, maarufu kama Samia Kalamu Awards kwa mwaka 2026.

Takwimu hizo zimetolewa Juni 17,2026 katika taarifa iliyosainiwa kwa pamoja kati ya mwenyekiti wa tuzo hizo Peter P. Mwasalyanda na Dkt. Rose Reuben ambaye ni mwenyekiti mwenza.

Katika taarifa hiyo imeandikwa pia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), wanaendelea kupokea kazi hizo huku takwimu zikionyesha kuwa kazi 569 (asilimia 91.2) ziko kwenye makundi ya tuzo za kisekta, kazi 25 (asilimia 4.0) kwenye tuzo maalumu za kitaifa, na kazi 20 (asilimia 4.8) zikiwa katika kundi la tuzo za vyombo vya habari.

Katika uwasilishaji huo, vyombo vya habari vya mtandaoni vimeibuka kidedea kwa kuwa vinara baada ya kuwasilisha kazi 276, ambayo ni sawa na asilimia 44 ya kazi zote zilizopokelewa hadi sasa.

Upande wa majukwaa mengine ya habari unaonyesha kuwa magazeti yamefuatia kwa kuwasilisha kazi 178 (asilimia 29), yakifuatiwa na televisheni zenye kazi 102 (asilimia 16), redio zikiwa na kazi 60 (asilimia 10), wakati majarida yakifunga orodha hiyo kwa kuchangia kazi 8 pekee ambayo ni sawa na asilimia 1 ya maombi yote.

Mwitikio huu mkubwa unaonyesha wazi jinsi matumizi ya majukwaa ya kidijitali yanavyozidi kushika kasi katika uzalishaji na usambazaji wa habari za maendeleo, huku ukionyesha dhamira thabiti ya wanahabari nchini katika kuelimisha na kuhamasisha jamii.

Kamati ya maandalizi imewapongeza wote waliowasilisha kazi zao na kuwasihi wale ambao hawajamaliza mchakato huo kutumia vyema muda uliosalia kabla ya dirisha kufungwa rasmi tarehe 30 Juni 2026 saa 5:59 usiku, ambapo kazi zinazokubaliwa ni zile tu zilizochapishwa au kurushwa kuanzia tarehe 1 Julai 2025 hadi tarehe 30 Juni 2026.

Tuzo za Samia Kalamu zilianzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2025 kufuatia ahadi na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyetaka ziwe mchakato endelevu wa kila mwaka, jambo ambalo alilisisitiza tena wakati wa ufunguzi wa Bunge la 13 tarehe 14 Novemba 2025.

 Chini ya kaulimbiu "Kalamu kwa Maendeleo", jukwaa hili la kitaifa linalenga kutambua na kuhamasisha weledi, maadili, utafiti na ubunifu katika uandishi wa habari zinazochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii, huku waandaaji wakiwakaribisha wadau mbalimbali kushirikiana nao kwa hali na mali kufanikisha hafla ya utoaji tuzo inayotarajiwa kufanyika kati ya mwezi Oktoba na Desemba 2026.

 

No comments