SERIKALI YAPOKEA GAWIO LA TRILIONI 1.3 KUTOKA KWA TAASISI ZA UMMA NA KAMPUNI
SERIKALI imepokea Sh trilioni 1.327 za gawio na michango mingine kutoka taasisi za umma na kampuni ambazo ina umiliki wa hisa chache.
Kiasi hicho ni sawa na ongezeko la asilimia 30 ikilinganishwa na Sh trilioni 1.028 za gawio la mwaka jana.
Msajili
wa Hazina, Nehemiah Mchechu alisema hayo katika hafla ya Gawio 2026 Ikulu ya
Dar es Salaam leo.
Alisema kiasi hicho kilichokusanywa hadi Juni 29, mwaka huu
ni ongezeko la Sh bilioni 299 kutoka makusanyo ya mwaka uliopita.
Mchechu
alisema kati ya fedha hizo, Sh bilioni 800.5, sawa na asilimia 60 ya makusanyo
yote zimetokana na gawio kutoka mashirika na kampuni za biashara, Sh bilioni
406 (asilimia 30) ni michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi kutoka taasisi
zisizo za kibiashara, huku Sh bilioni 121.5 (asilimia 10) zikitokana na mapato
mengine yanayohusiana na uwekezaji wa serikali.
Alisema
katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, makusanyo ya gawio na michango
yameongezeka kutoka Sh bilioni 637 mwaka 2020/2021 hadi Sh trilioni 1.327 mwaka
2025/2026, sawa na ukuaji wa asilimia 108.
Aidha,
Mchechu alisema thamani ya uwekezaji wa serikali unaosimamiwa na Ofisi ya
Msajili wa Hazina imeongezeka kutoka Sh trilioni 67.01 mwaka 2020/2021 hadi Sh
trilioni 92.2 mwaka 2024/2025, sawa na ongezeko la asilimia 37.
Alisema
mafanikio hayo yamechangiwa na kuimarika kwa utawala bora, uwajibikaji,
matumizi ya teknolojia, uwekezaji wa kimkakati na usimamizi madhubuti wa mali
za umma.
“Taasisi
hizi zimekumbatia mageuzi ya kiuongozi na kibiashara na zimeendelea kujijenga
upya ili ziweze kutoa matokeo makubwa zaidi kwa taifa,” alisema Mchechu.
Alitoa
mfano kuwa baadhi ya mashirika yaliyokuwa yakikabiliwa na changamoto za kifedha
sasa yameanza kurejea katika faida.
Alitaja
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) lililopata faida ya Sh bilioni 22.9
mwaka 2024/2025 baada ya kupata hasara ya Sh bilioni 18 mwaka uliotangulia na
hivyo kutoa gawio la Sh bilioni 1.6 kwa serikali.
Pia,
alisema Shirika la Posta Tanzania limepata faida ya Sh bilioni 2.8 baada ya
kutoka kwenye hasara ya Sh bilioni 27.9, huku Shirika la Madini la Taifa
(STAMICO) likiendelea kupata faida ya Sh bilioni 20.5 na kuendelea kutoa gawio
kila mwaka.
Kwa
upande wa huduma za umma, alisema Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI)
imefanikiwa kuwafanyia upasuaji mkubwa wa moyo zaidi ya wagonjwa 760 kwa
kutumia uwekezaji na ruzuku ya serikali ya Sh bilioni 6.7, hatua iliyopunguza
rufaa za matibabu nje ya nchi na kuokoa fedha za kigeni.
Aidha,
alisema Hospitali ya Benjamin Mkapa imeendelea kufanya upandikizaji wa figo na
uloto kwa wagonjwa wa selimundu, wakati Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa
(NIDA) imeendelea kuwa mhimili wa uchumi wa kidijiti na mwaka huu imewasilisha
gawio la Sh bilioni 61 kwa serikali.
Mchechu
alisema serikali pia imeendelea kupanua umiliki wake katika sekta ya madini
ambapo idadi ya miradi ambayo serikali ina hisa kupitia Msajili wa Hazina
imeongezeka kutoka 10 hadi 15 kufikia Juni 2026 na mingine 10 ipo hatua za
mwisho za majadiliano.
Alisema
kampuni ambazo serikali ina hisa, zikiwemo NMB Bank, NBC Bank, TAZAMA
Pipelines Limited, Puma Energy Tanzania, TPC Limited, Mbeya Cement Company
Limited na Airtel Tanzania, zimeendelea kuongeza faida, thamani ya
uwekezaji na gawio kwa serikali.






Post a Comment