Balozi wa Italia Akoshwa na Ngoma ya Wahadzabe ZIFF 2026
Msisimko wa ufunguzi wa msimu wa 29 wa Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF 2026) ulipanda joto pale Balozi wa Italia nchini Tanzania, Mheshimiwa Giuseppe Sean Coppola, pamoja na viongozi wakuu wa tamasha hilo waliposhindwa kuzuia hisia zao na kuingia kilingeni kucheza ngoma ya jadi.
Tukio hilo lilitokea baada ya kuwepo kwa burudani ya kipekee na ya kuvutia kutoka kwa jamii ya asili ya Wahadzabe, onyesho ambalo liliteka hisia za watazamaji zaidi ya 300 waliokuwa wakifuatilia kwa karibu tamasha hilo la kihistoria.
Kabla ya kuingia rasmi kwenye ngoma yenyewe, jamii hiyo ilitawala jukwaa kwa mchezo wa kuigiza uliotengeneza taswira halisi ya maisha yao ya kila siku ya nyumbani na harakati za uwindaji.
Taswira hiyo ya asili ilikuwa ya kuvutia mno na iliwaacha watazamaji wengi wakiwa wamebaki vinywa wazi kwa mshangao na msisimko mkubwa kutokana na uhalisia uliokuwa ukitiririka jukwaani.
Baada ya kuonesha tamaduni hizo za maisha ya kawaida, burudani hiyo iligeuka kuwa sherehe kubwa na ya kihistoria pale Wahadzabe walipoanza kushangilia maisha yao kupitia miondoko ya ngoma ya jadi ambayo ni nadra sana kuishuhudia nje ya mazingira yao ya asili.
Ilikuwa ni midundo ya kusisimua iliyosababisha jukwaa zima kutikisika kwa nguvu ya miguu yao, huku hewa ikijazwa na mikono iliyokuwa ikitinga kwa madaha, hali iliyomvutia Balozi Coppola na viongozi wa ZIFF kuruka jukwaani na kujumuika nao katika kushangilia tamaduni hiyo adhimu.

Post a Comment